Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aliyembaka dada wa kazi badala ya kumsitiri atupwa jela miaka 30

43cbec2e68cd684e82c5ff76af193d44 Aliyembaka dada wa kazi badala ya kumsitiri atupwa jela miaka 30

Wed, 16 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza imemuhukumu kwenda jela miaka 30, Edward Machibya, mkazi wa mtaa wa Buduku, Kata ya Kiseke wilayani humo baada ya kukutwa na kosa la kumbaka dada wa kazi (Jina limehifadhiwa).

Akitoa hukumu hiyo hivi karibuni, Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Phortunatus Kubaja alieleza kuwa mtuhumiwa Machibya mwenye miaka zaidi ya 40 alitenda kosa hilo Februari 13 mwaka huu.

Ilielezwa mahakamani hapo kuwa kwa kutumia nguvu Machibya alimuingilia kimapenzi dada huyo wa kazi mwenye umri wa miaka 15 na kumsababishia maumivu makali sehemu zake za siri na kusababisha kutokwa na damu nyingi.

Hakimu Kubaja aliieleza mahakama kuwa ushahidi uliotolewa umeonesha chanzo cha tukio hilo ni binti huyo ambaye alikuwa anafanya kazi za ndani kukosa sehemu ya kulala usiku wa Februari 12, mwaka huu kutokana na kile kinachodaiwa kutofautina na mwajiri wake.

Ilipofika saa 5:00 usiku aliamua kutafuta msaada kwa mama Misuji Simoni ambaye ni rafiki wa mwajiri wake.

Baada ya binti huyo kufika, mama Misuji alielekeza binti apelekwe kwa Mwenyekiti wa mtaa akisindikizwa na wanaume wawili ambao ni watu wa karibu na mumewe akiwemo mtuhumiwa.

Wakati wakielekea kwa Mwenyekiti wa mtaa, Machibya ambaye ni mtuhumiwa alipendekeza aende na binti huyo nyumbani kwake na alipofika alihitaji kufanya naye mapenzi ili ampe sehemu ya kulala, alipokataa kwa kutumia nguvu mtuhumiwa alimfunga mikono na kutenda kosa hilo.

Hakimu alieleza kuwa kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na Jeshi la Polisi kwa kesi hiyo ya jinai namba 30 ya mwaka 2020, umebainisha mtuhumiwa alihusika kutenda kosa hilo na hivyo amekutwa na kesi ya kujibu ambapo kwa mjibu wa sheria, baada ya mahakama kujiridhisha na ushahidi uliotolewa na kusikiliza upande wa utetezi imemuhukumu mtuhumiwa huyo kwenda jela miaka 30.

Aidha Machibya alipatiwa nafasi ya kujitetea mbele ya mahakama ambapo alikana kutenda kosa hilo kwa madai kilichosababisha atuhumiwe kuhusika na tukio hilo ni kutokana na ugomvi aliokuwepo kati yake na Mwenyekiti wa mtaa, utetezi ambao ulitupiliwa mbali na Mahakama na hakimu aliamuru hukumu hiyo kutekelezwa kama ilivyosomwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la WoteSawa linalojishughulisha kutetea haki za wafanyakazi wa majumbani , Angela Benedicto akizungumzia hukumu hiyo jana alisema kama wanaharakati wanafarijika kuona haki inatendeka na watuhumiwa wa matukio ya ukatili dhidi ya wafanyakazi wa majumbani wanachukuliwa hatua stahiki.

Angela alisema ni vyema pia waajiri wa wafanyakazi wa majumbani wawajibike kupinga aina yeyote ya ukatili kwani kwa matukio mengi yanayotokea wao ndiyo wamekuwa chanzo na iwapo hakuna maelewano baina ya mwajiri na mwajiriwa ni vyema mwajiri awajibike kumrejesha mfanyakazi wake hadi nyumbani alipomtoa, badala ya kumfukuza ili kuepusha kumuweka katika mazingira hatarishi binti huyo.

Chanzo: habarileo.co.tz