Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aliyekuwa msaidizi wa Sabaya alivyotoa siri kwa Mbowe

Mbowe 0 (1) Aliyekuwa msaidizi wa Sabaya alivyotoa siri kwa Mbowe

Thu, 28 Oct 2021 Chanzo: ippmedia.com

MSAIDIZI wa zamani wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, Justine Kaaya, amedai alikutana na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, mara tatu na kumpa majina manane na namba za simu za marafiki wa Sabaya, akaahidi kushughulika nao.

Kaaya pia amedai alimtajia Mbowe klabu nne ambazo Sabaya alipenda kutembelea na hoteli tatu alizokuwa analala.

Shahidi huyo wa pili wa upande wa mashtaka alidai hayo jana Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi mbele ya Jaji Joackim Tiganga.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Abdallah Chavule, alidai alikuwa anafanya kazi na Sabaya tangu mwaka 2017 akiwa Diwani wa Kata ya Sambasha wilayani Arumeru, akipiga picha zake pamoja na viongozi wengine akiwamo aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.

Alidai alikuwa na kazi ya kupiga picha katika uchaguzi mdogo Jimbo la Longido na Sabaya alitaka amsaidie kupiga picha kwenye kata yake, alikubali akahama Longido kwenda Arusha nyumbani kwa Sabaya, eneo la Kibanda Maziwa, Sakina.

Alidai Sabaya alikuwa akiishi na mkewe Jesca katika nyumba hiyo na aliishi humo hadi Julai 2018, Sabaya alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai.

"Nilienda kuishi na Sabaya katika makazi ya DC, Hai, nilikuwa msaidizi wake katika shughuli ndogo ndogo, kunyoosha nguo, kupeleka chai na chakula ofisini kila siku.

"Niliishi kwa Sabaya hadi Oktoba 2018 nikaamua kuacha kazi, nikarudi Longido kusimamia kazi zangu na niliacha mchumba.

"Novemba 2018 nilipigiwa simu na Mbowe kupitia namba yake 0784779944, alijitambulisha na kuomba tuonane, alisema yuko Arusha, nilimwambia niko Longido kuna changamoto ya usafiri.

"Aliniambia nichukue Noah atalipa gharama nikifika Arusha lakini nilikataa kwa sababu ya hofu, alikata simu, baada ya muda akapiga na kusema yuko njiani anakuja Longido.

"Baada ya dakika 40, alinipigia kafika yuko uwanja wa mpira, nilienda kwa bodaboda, nikakuta gari, nikampigia akaniambia nisogee kwenye gari, nilipofika niligonga kioo, akashusha na kuniambia niingie ndani ya gari nisiwe na wasiwasi.

"Niliingia siti ya nyuma, ndani alikuwa Mbowe na dereva mwanamke, alisema Lengai anamsumbua, akataka nimpe taarifa za kazi anazofanya Sabaya na watu wake wa karibu alionao Hai.

"Nilimwambia haiwezekani sipo kwa Sabaya, alisema yeye kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini, atafanya namna yoyote anayoweza ili nirudi kuendelea na kazi kwa Sabaya," alidai Kaaya.

Alidai alimwambia Mbowe hawezi kurudi kwa Sabaya, alichagua kufanya shughuli zake binafsi na Mbowe alimwomba msamaha kwa kumsumbua, akampa Sh.300,000, akasema watawasiliana.

"Nilimpigia Sabaya simu kumpa taarifa lakini hakupokea, nilimpigia Mbunge wa Longido, Dk. Steven Kiruswa, nilimweleza yote aliyoongea Mbowe, nikarudi nyumbani.

"Mbowe alinipigia tena Januari 2020 kwa WhatsApp kupitia namba zake, akataka tuonane Moshi, nilienda Moshi, akanielekeza nishuke Machame Road, nikae upande wa kulia, akaja na gari aina ya Land Cruser V8 yenye mlingoti na bendera ya Bunge, namba za gari zilikuwa KUE.

"Alishusha kioo cha gari akaniambia ingia kwenye gari, nyuma akashuka mtu mmoja akaniambia nipite, niliingia kwenye gari na baada ya dakika nane tulifika Aishi Hoteli Machame.

"Mbowe na mlinzi wake tulienda kukaa upande wa mgahawa, akataka tuzungumze muda mfupi, wana mkutano ndani ya jimbo, aliniruhusu niagize kinywaji au chakula, ilikuwa saa saba mchana.

"Aliniomba nimtajie rafiki zake Sabaya aliokuwa nao Hai, nilimtajia majina yao na namba za simu.

"Nilimtajia Japhet Bendera, Renatus Sibula, Mtoto wa Mkulima, Silveter Nyegu, Binti wa Kichaga, Mwalimu Dorine, Watson Malimwengu na Enock Kirigiti.

"Alisema atashughulika nao, akasema atanitumia chochote kwenye simu lakini hakufanya hivyo nikaamua kurudi Arusha, Julai mwaka 2020 alinipigia kwa WhatsApp akasema saa moja usiku atakuwa Moshi niende.

"Nilienda tukakutana Keys Hoteli, nilikuwa na dereva wake Willy pamoja na mlinzi wake baunsa baunsa, tulimsubiri alipotoka kwenye kikao tulielekea kwenye gari tukiwa naye pamoja na Mbunge wa Viti Maalum, Joyce Mukya," alidai.

Shahidi huyo alidai walienda Aishi Hotel, Mbowe akamwambia Joyce atangulie chumbani, wao wana kikao kifupi.

"Mbowe alijitambulisha mlinzi wake na msiri wake anaitwa Halfani Bwire, alisema niwe huru kuzungumza naye, alitaka majina ya rafiki wa Sabaya, nilimwandikia, alitaka nimwandikie klabu anazotembelea Sabaya na hoteli anazolala.

"Nilimwandikia Klabu ya Kokoliko Anex , Kokoliko, Zedone iliyopo maeneo ya TBL, Arusha, Main Stone Park iliyopo Sakina na hoteli ya SG Resort, Kamau Hotel na Empress Hotel.

"Nilimuuliza anafanyia kazi gani, akajibu nimwachie yeye, alisema kazi yangu imeisha. Nilimkabidhi Bwite karatasi niliyoandika, Bwire akasema Sabaya mtoto mdogo sana.

"Mbowe alisema kazi imeanza rasmi ataanza kunilipa mshahara, muda ulikuwa umeenda, nilipewa chumba nikalala Aishi Hotel, asubuhi alinitumia Sh. 200,000 kwenye simu yangu ya voda namba 0754 916666, nilirudi Arusha saa 12 asubuhi," alidai.

Kaaya alidai hakuwasiliana tena na Mbowe tangu siku hiyo hadi alipokamatwa Agosti 25 mwaka 2020 kwa tuhuma za kula njama kufanya vitendo vya kigaidi na kutakatisha fedha.

Alidai aliunganishwa katika kesi na Bwire, Adamu Kasekwa na Mohammed Ling'wenya, alikuwa akimfahamu Bwire sababu alikutana naye Aishi Hotel na Keys akiwa na Mbowe.

"Nilikaa gerezani miezi 11, Julai 26 mwaka 2021 aliletwa Mbowe gerezani Ukonga, alinikuta na Bwire, alituambia poleni sana nimekuja kuwatoa.

"Julai 27, 2021 tulipelekwa Mahakama ya Kisutu upande wa Jamhuri wakasema hawana nia nikaachiwa huru, nilienda Kituo Kikuu cha Polisi kwa mpelelezi nikapewa vitu vyangu vyote ikiwamo fedha, simu na vitambulisho vyangu," alidai.

Alidai wakati anakamatwa, alikuwa akienda benki kuweka fedha Sh. 1,017,000 na Dola za Marekani 1,100.

Akihojiwa na Wakili wa Utetezi, Jeremiah Mtobesya, shahidi alikiri kutotoa uthibitisho wowote mbele ya mahakama kuthibitisha alifanya kazi na Sabaya.

Akihojiwa na Wakili John Mallya, shahidi alidai hafahamu diwani analipwa posho kiasi gani na hafahamu Sabaya alimlipa posho kutoka mfuko gani na hakujua anatoa wapi fedha hizo.

Anadai alikuwa analipwa Sh. 300,000 kwa mwezi na Sabaya kama posho yake na kwamba anajua Sabaya alikuwa na mke na hajui kama alidanganya kuwa ana mchumba.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Bwire, Adamu Kasekwa, Mohammed Ling'wenya na Mbowe wanaokabiliwa na mashtaka sita yakiwamo ya kula njama kufanya vitendo vya kigaidi kati ya Mei Mosi na Agosti 5 mwaka 2020 mikoa ya Morogoro, Arusha, Moshi, Dar es Salaam na Mwanza.

Chanzo: ippmedia.com