Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aliyekuwa mhasibu NHIF kortini, asomewa mashtaka 30

Nhif Pic Data Aliyekuwa mhasibu NHIF kortini, asomewa mashtaka 30

Wed, 3 Nov 2021 Chanzo: mwananchidigital

Aliyekuwa mhasibu msaidizi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) mkoa wa Mara, Francis Mchaki (37) amefikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka 30 likiwemo shtaka la uhujumu uchumi na kusababishia mfuko huo hasara ya zaidi ya Sh3.38 bilioni.

Mchaki amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mara pamoja na aliyekuwa meneja wa NHIF mkoa wa Mara, Dk Mgude Bachunya (51) na aliyekuwa msimamizi wa mfuko huo mkoa wa Mara, Dk Leonard Mitti (51).

Watuhumiwa hao kwa pamoja na watu wengine ambao bado hawajafikishwa mahakamani wanadaiwa kutenda makosa hayo kwa nyakati tofauti kati ya Januari 2013 hadi Machi 2016 ambapo wakati mhasibu huyo msaidizi anashtakiwa kwa makosa 30, Dk Bachunya akishtakiwa kwa makosa 20 huku Dk Mitti akishtakiwa kwa makosa 11.

Wakili wa Serikali, Tawabu Issa ameelea mbele ya hakimu mkazi mwandamizi wa mahakama hiyo, Eugenia Rujwahuka kuwa miongoni mwa makosa wanayoshtakiwa nayo mbali na kosa la uhujumu uchumi ni pamoja na matumizi mabaya ya ofisi na matumizi mabaya ya madaraka huku wakiwa ni watumishi wa umma.

Makosa mengine ni kuisababishia hasara mfuko wa bima ya afya, kugushi nyaraka mbalimbali kwa lengo la kumdanganya mwajiri, kutumia nyaraka za uongo pamoja na ufujaji wa pesa za umma.

Hata hivyo baada ya kusomewa mashtaka hayo, hakimu Rujwahuka amesema kuwa mahakama hiyo haina mamalaka kisheria kusikiliza kesi hiyo hivyo kuamuru watuhumiwa hao kupelekwa mahabusu huku taratibu zikifanyika kati ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) pamoja na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa hatua zaidi.

"Ingawa dhamana iko wazi lakini mahakama hii kama nilivyoeleza hapo awali haina mamlaka ya kutoa dhamana hivyo mtapelekwa rumande lakini mnaweza kuanza mchakato wa kuomba dhamana kupitia Mahakama Kuu muda wowote na mkitimiza masharti mtapewa hiyo dhamana kwa sasa mnapelekwa mahabusu hadi Novemba 15 mwaka huu kesi hii itakapoletwa tena hapa" amesema.

Chanzo: mwananchidigital