Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, imemkuta na kesi ya kujibu, aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (Rahco), Benhardard Tito.
Tito amekutwa na kesi ya kujibu baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wao wa mashahidi tisa waliyowasilisha mahakamani hapo kuthibitisha mashtaka.
Wakati Tito amekutwa na kesi ya kujibu, washtakiwa wenzake Emmanuel Massawe aliyekuwa mwanasheria wa kampuni hiyo na mwakilishi wa kampuni ya Rothschild (South Africa) Proprietary Limited, Kanji Mwinyijuma, wameachiwa huru na mahakama hiyo, baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yao.
Tito na wenzake wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 12/2016 yenye mashtaka nane likiwemo la kuisababishia Serikali, hasara ya dola za kimarekani 527, 540, sawa na Sh 1.2bilioni.
Uamuzi huo imetolewa leo na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rhoda Ngimilanga wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutolewa uamuzi, iwapo washtakiwa hao wanakesi ya kujibu au laa.
Hakimu Ngimilanga amesema mshtakiwa Tito amekutwa na kesi ya kujibu baada ya ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo na upande wa mashtaka, hivyo anatakiwa kujitetea.
"Mahakama hii pia imewaona Massawe na Mwinyijuma hawana kesi ya kujibu kwani ushahidi wote ulioletwa na Jamhuri haujawaonyesha nyie kuwa na kesi ya kujibu, hivyo Mahakama hii nawaachia huru kuanzia Sasa" amesema Hakimu Ngimilanga.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Ngimilanga ameahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 13, 2022 ambapo itaitwa kwa ajili ya Tito kuanza kujitetea.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wadaiwa kati ya Septemba Mosi, 2014 na Septemba 30, 2015, Wanadaiwa kutenda kosa la kula njama kinyume cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa.
Miongoni mwa mashtaka hayo, Tito, anadaiwa kuwa Februari 27, 2015 katika ofisi za Rahco zilizopo Ilala alitumia madaraka yake vibaya kwa kuiajiri Kampuni ya Rothschild (South Africa) Proprietary Ltd kama mshauri wa mradi wa uimarishaji wa reli ya kati, bila idhini ya Bodi ya Rahco.