Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aliyekuwa DED Rombo, kortini kwa uhujumu

38187 DED+PC Aliyekuwa DED Rombo, kortini kwa uhujumu

Thu, 24 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Vigogo wawili wa zamani wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, wamepandishwa kizimbani mjini Moshi wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kwa kuisababishia Serikali hasara ya Sh226.6 milioni.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, vigogo hao ni aliyekuwa mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Judethadeus Mboya na aliyekuwa mwanasheria, Andrew Gregory.

Washtakiwa hao walifikishwa kortini jana mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Moshi, Bernazitha Maziku na kusomewa mashtaka mawili na mwendesha mashtaka wa Takukuru, Suzy Kimario.

Kimario alidai kuwa Desemba 2013, washtakiwa hao walitumia madaraka yao vibaya kwa kuandaa mkataba mbaya.

Alidai kuwa watumishi hao waliandaa na kusaini mkataba kabla ya majadiliano kati ya halmashauri na kampuni ya Jun Yu Investment International iliyojenga kiwanda cha Moshi Cement kilichopo Holili wilayani Rombo.

Kosa la pili, alidai kuwa waliisababishia halmashauri hasara ya Sh226.6 milioni, kosa ambalo linaangukia chini ya Sheria ya Uhujumu uchumi kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 28 baada ya upande wa mashtaka kueleza kuwa upelelezi haujakamilika na washtakiwa walirejeshwa rumande hadi siku hiyo.



Chanzo: mwananchi.co.tz