Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aliyekutwa na kadi 20 za ATM apandishwa kizimbani

89419 ATM+PIC Aliyekutwa na kadi 20 za ATM apandishwa kizimbani

Fri, 20 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkazi wa Chalinze, mkoani Pwani nchini Tanzania, Halima Juma Ally, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam akikabiliwa na mashtaka matatu ya wizi wa kimtandao. 

Halima mwenye umri wa miaka 23, aliyetiwa mbaroni na jeshi a Polisi akidaiwa kukutwa na kadi zaidi ya 20 za benki zinazotumika kutolea fedha kwenye mashine ya ATM, amepandishwa kizimbani mahakamani hapo na kusomewa mashtaka yanayomkabili, leo Ijumaa, Desemba 20, 2019. 

Akimsomea mashtaka yanayomkabili, Wakili wa Serikali Kamugisha Gabriel ameieleza mahakama katika shtaka la kwanza mshtakiwa aliiba kadi hiyo ya ATM ya CRDB, mali ya Ernest Sakwa. 

Wakili Gabriel amedai mshtakiwa alitenda kosa hilo Oktoba 23, 2019, eneo la Mbagala, wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam. 

Katika shtaka la pili, wakili Gabriel amedai  katika tarehe hiyohiyo, mshtakiwa aliiba Sh2,050,000 eneo la Mtoni kwa Aziz Ali, Temeke jijini Dar es Salaam, mali ya Sakawa. 

Pia, wakili Gabriel katika shtaka la tatu amedai tarehe hiyohiyo mshtakiwa aliiba Sh2 milioni, mali ya Sakawa na kwamba alitenda kosa hilo eneo la Keko Bara, Temeke jijini Dar es Salaam. 

Hata hivyo mshtakiwa alipoulizwa likana kutenda makosa hayo yote. 

Wakili Gabriel ameeleza mahakama upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na akaiomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

 

Aliieleza mahakama kuwa upande wa mashtaka hauna pingamizi la dhamana dhidi ya mshtakiwa kwa kuwa mashaka yanayomkabili yanadhaminika. 

Hata hivyo, aliiomba mahakama hiyo itoe masharti ambayo yatawezesha mshtakiwa kupatikana na kufika mahakamani kila atakapohitajika kwa kuzingatia kuwa si mkazi wa Dar es Salaam. 

Hakimu Godfrey Rwekiti anayesikiliza kesi hiyo alimtaka mshtakiwa huyo kuwa na wadhamini wawili wanaotambulika ambao watasaini bondi ya Sh2 milioni kila moja. 

Hata hivyo, alishindwa kutimiza sharti hilo kwa hakuwa na wadhamini na hakimu Rwekiti aliamuru apelekwe mahabusu hadi Desemba 30, 2019 kesi yake itakapotajwa tena. 

Novemba 23, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema  mwanamke huyo alikamatwa katika benki ya CRDT tawi la Mbagala na askari aliyekuwa zamu baada ya kumtilia shaka. 

Alisema mwanamke huyo alikuwa akijifanya kuwasaidia wazee  ndani ya chumba cha mashine ya fedha katika benki hiyo, lakini kumbe alikuwa na lengo la kuchukua namba zao za siri na kisha kuwabadilishia kadi hizo na kuwapa kadi bandia alizokuwa nazo. 

Chanzo: mwananchi.co.tz