Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aliyekutwa na jongoo bahari ahukumiwa faini ya Sh200,000

Jongoo Jongoo Aliyekutwa na jongoo bahari ahukumiwa faini ya Sh200,000

Tue, 18 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemhukumu raia wa China, Wei Zhang (54) kulipa faini ya Sh 200, 000 ua kwenda jela mwaka mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na jongoo bahari (Sea Cucumber), walio hatarini kutoweka, wenye uzito wa kilo 4.10.

Pia mahakama hiyo imetaifisha jongoo hao na kuwa mali ya Serikali, ambapo watarejeshwa kwa mamlaka husika.

Hukumu hiyo imetolewa leo Jumanne, Julai 18, 2023 na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutolewa hukumu.

Zhang ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Kinondoni, alikiri shtaka lake wiki mbili zilizopita, wakati aliposomewa hoja za awali (PH).

Hata hivyo, leo Hakimu Shaidi amesema mahakama hiyo imemtia hatiani mshtakiwa kama alivyoshtakiwa, hivyo anatakiwa kupewa adhabu.

“Mshtakiwa amekubali shtaka lake na mahakama hii imemtia hatiani kama alivyoshtakiwa, hivyo inampa adhabu," amesema Hakimu Shaidi na kuongeza;

"Kwa kuwa mshtakiwa ni mkosaji wa mara ya kwanza, mahakama hii inakupiga faini ya Sh 200,000 na ukishindwa, utatumikia kifungo cha mwaka mmoja jela," amesema Hakimu Shaidi.

“Pia Mahakama hii inataifisha majongoo haya na kuwa mali ya Serikali" anasem hakimu Shaidi.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Mahakama hiyo ilitoa nafasi kwa mshtakiwa kujitetea kwanini asipewe adhabu kali.

Hata hivyo mshtakiwa huyo aliomba apunguziwe adhabu kwa kuwa ni kosa lake la kwanza na alikuwa hajui kama kuna sheria inayokataza kumiliki Jongoo hao.

“Mheshimiwa hakimu naomba mahakama yako inipunguzie adhabu kwa kuwa mimi ni mkosaji kwa mara ya kwanza, na niliuziwa na mtu wala sikwenda kutafuta hawa Jongoo bahari, hivyo sikufanya makusudi naomba nipunguzie adhabu," amedai mshtakiwa.

Awali, Wakili wa Serikali, Tumaini Maingu akiiomba Mahakama itoe adhabu kali dhidi ya mshtakiwa huyo kwa kuwa viumbe hao walipo hatarini kutoweka.

“Upande wa mashtaka hatuna kumbukumbu za makosa ya nyuma kama alishawahi kushtakiwa mahakamani hapa, lakini naomba mahakama yako itoa adhabu kali kwa mujibu wa sheria," amedai Maingu.

Maingu amedai kuwa kwa mshtakiwa ambaye akikutwa na hatia kwa mara ya kwanza kwa kosa hilo, adhabu yake ni faini isiyopungua Sh 200,000 na isiyozidi Sh1 milioni au kifungo kisichopungua miaka miwili na kisichozidi miaka mitano au adhabu zote kwa pamoja.

“Hivyo naomba Mahakama yako izingatie adhabu kwa mujibu wa sheria "amedai Wakili Maingu.

Katika kesi ya msingi, mshtakiwa alikuwa anakabiliwa na kesi ya jinai namba 113/2023.

Anadaiwa kutenda kosa hilo April 7, 2023 katika Mtaa wa Kumbukumbu uliopo Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Siku hiyo ya tukio, mshtakiwa huku akijua jamii hiyo ya Jongoo bahari ipo hatarini kutoweka, alikutwa akiwa na kilo 4.10 za Jongoo hao kinyume cha sheria.

Zhang kwa mara ya kwanza, alifikishwa mahakamani hapo Juni 26, 2023 na kusomewa kesi hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live