Dar es Salaam. Hany Ahmed (27), raia wa Misri amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na shtaka la kutorosha madini ya almasi yenye thamani ya zaidi ya Sh12 milioni.
Ahmed amefikishwa mahakamani hapo leo Jumanne Julai 16, 2019 na kusomewa shtaka na wakili wa Serikali mwandamizi, Wankyo Simon.
Simon amedai mshtakiwa anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Thomas Simba, Simon amesema mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo Julai 10, 2019 Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam.
Siku ya tukio, Ahmed alikutwa akisafirisha madini hayo yenye uzito wa carats 11:12 ambayo yana thamani ya dola za Marekani 5,238 sawa na Sh12, milioni bila ya kuwa na kibali kutoka mamlaka husika.
Baada ya kusomewa shtaka hilo, raia huyo wa Misri hakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.
Pia Soma
- Bongo movie, Swahilflix kumleta Will Smith Tanzania
- Rais Magufuli asisitiza bei elekezi zao la pamba ni Sh1,200
- NEC kuanza uboreshaji wa Daftari, Kihamia atoa mwongozo
- TCU yavifungulia vyuo vilivyofungiwa kudahili
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 30, 2019 itakapotajwa tena na mshtakiwa kurejeshwa rumande.