Mahakama ya Rufani imemwachia huru mwanamke mkazi wa Moshi, Luthgnasia Mushi, ambaye mwaka 2019 alihukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kupatikana na hatia ya kusafirisha misokoto 234 ya bangi.
Luthgnasia alikamatwa na polisi Aprili 24, 2014 saa 10:15 alasiri nje ya Kituo cha Polisi cha Usalama Barabarani mjini Moshi akidaiwa kuwa na begi dogo la rangi ya kahawia likiwa na dawa hizo za kulevya.
Siku hiyo, Inspekta Bernard Kapusi alifuatwa na mtu aitwaye Constantine Masumbuko, aliyemtonya kuwa mwanamke huyo aliyekuwa akipita nje ya Kituo Kikuu cha Polisi alikuwa amebeba begi lenye bangi.
Kwa kusaidiana na WP Bakita, walimfuata mwanamke huyo na kumkamata katika geti la Kituo cha Usalama Barabarani na kumpeleka Kituo Kikuu kumfanyia upekuzi, ndipo alikutwa na misokoto hiyo.
Katika utetezi wake, mshtakia huyo alikana kukamatwa nje ya Kituo cha Polisi kama ilivyodaiwa na polisi bali alikamatwa Soko Kuu na hakuwa na dawa hizo za kulevya, hivyo akahusisha kukamatwa kwake na mchezo mchafu uliosukwa na Masumbuko.
Alieleza kuwa Masumbuko ambaye aliwahi kuwa mpenzi wake aliahidi kumkomesha baada ya kubeba mimba ya mwanamme mwingine wakati Masumbuko akiwa gerezani kwa kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha.
Hata hivyo, baada ya kusikiliza mashahidi wa upande wa mashtaka na utetezi, Mahakama ya Hakimu mkazi Moshi ikiwa na mamlaka ya nyongeza ya kusikilisha shauri hilo, ilisema upande wa mashtaka umethibitisha mashtaka na ikamtia hatiani.
Mashatkiwa hakuridhika na hukumu hiyo iliyotolewa na Joachim Tiganga, hakimu mkuu mkazi mfawidhi ambaye sasa ni Jaji wa Mahakama Kuu, akisema kifungo kilikuwa batili kikatiba na pia upande wa mashtaka haukuthibitisha mashtaka dhidi yake.
Jopo la majaji watatu, Jacob Mwambelege, Patricia Fikirini na Abraham Mwampashi katika hukumu yao waliyoitoa Agosti 25, walikubaliana na baadhi ya sababu za rufaa za mwanamke huyo na kumuachia huru.
Katika hukumu hiyo, majaji hao lilikubaliana na hoja za mrufani kuwa kulikuwa na kujikanganya, mapungufu na ushahidi usio na mtiririko.
Alisema kama si kuibua hoja hiyo, wangeweza kuiona rufaa haina mashiko.
Pia majaji hao walisema kama si kushindwa kwa upande wa mashtaka kumuita Masumbuko ambaye ni shahidi muhimu hasa katika mazingira ambayo mrufani anasema ndiye alimtengenezea kesi, hoja hiyo isingekuwa na mashiko.
“Haiko wazi katika ushahidi kwanini mrufani hakupekuliwa mahali alipokamatiwa. Wala hauelezw kwanini hakupelekwa Kituo cha Polisi cha Trafiki ambacho kipo hatua 15 tu lakini wakaamua kwenda Kituo Kuu cha Polisi,” imehoji hukumu hiyo.
Hoja ya pili kwa mujibu wa majaji, ni hatua ya upande wa mashtaka kushindwa kumuita Masumbuko kama shahidi wakati ndiye anayetajwa na shahidi wa pili kuwa ndiye aliyemweleza kuwa mwanamke huyo alikuwa na begi lenye bangi.
Kuhusu hoja ya kwamba adhabu aliyopewa ilikiuka Katiba, majaji hao walisema wanaipuuza kwa kuwa mahakama hiyo haikuketi kama mahakama ya kikatiba, hivyo wanamwachilia huru kwa sababu nyingine ambazo walizieleza.