Dar es Salaam. Mshtakiwa James Stephano (24) anayetumikia kifungo cha miaka 20 jela kwa kubaka, Julai 3, 2019 ataanza kujitetea katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala Dar es Salaam katika kesi nyingine ya kubaka watoto wawili wa kike wenye umri wa miaka sita na tisa.
Stephano ambaye alikwisha hukumiwa kifungo cha miaka 20 jela na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Samwel Obasi katika kesi nyingine ya kubaka, siku hiyo ya Julai 3, 2019 ataanza kujitetea katika kesi ya jinai namba 109 ya mwaka 2018 ambayo inasikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi, Flora Mujaya na Wakili wa Serikali, Aziza Muhina.
Mshtakiwa huyo alipaswa kuanza kujitetea leo Alhamisi Juni 20, 2019 lakini ilishindikana baada ya Wakili wa Serikali Grace Lwila kueleza Mahakama hawajajiandaa hivyo ikasogezwa hadi Julai 3, 2019.
Katika kesi hiyo, Stephano anadaiwa kubaka watoto wawili wa kike kosa ambalo anadaiwa kulitenda kati ya Julai na Agosti mwaka 2017 huko Gongolamboto jijini Dar es Salaam.
Ilidaiwa mahakamani hapo kosa hilo ni kinyume na kifungu cha 130(1)(2)(e) na 131 (1) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Hatua hiyo ilifikiwa mahakamani hapo baada ya shahidi wa upande wa mashtaka ambaye ni askari kutoka kituo cha Polisi cha Stakishali, kitengo cha Dawati la jinsia na watoto, WP 5034 D/Koplo Zainabu kutoa ushahidi wake na lipomaliza upande wa mashtaka ukafunga kesi yao.
Pia Soma
- Mbunge CCM asema hali ya uzalishaji wa mazao ya biashara si nzuri
- Mkenya kortin kwa kusafirisha madini ya Sh500 milioni
- Mfanyabiashara kortin kwa kusafirisha dhahabu kinyume cha sheria
Hata hivyo, baada ya Hakimu Mujaya kutoa uamuzi huo alimuuliza mshtakiwa huyo kama atakuwa na mashahidi wangapi watakaotoa ushahidi upande wake naye alijibu atakuwa na shahidi mmoja aliyemtaja kwa jina la Ester.