Moshi. Aliyekuwa mshtakiwa wa kwanza, Hamis Chacha katika kesi ya mauaji ya mwanafunzi wa Scolastica, Humphrey Makundi (16), ameamua kukimbilia Mahakama ya Rufaa kupinga hukumu ya kifo.
Juni 3, Jaji Firmin Matogolo wa Mahakama Kuu, alimhukumu Chacha kunyongwa hadi kufa, huku washtakiwa wenzake wawili wakihukumiwa kifungo cha miaka minne jela kila mmoja.
Mbali ya Chacha ambaye alikuwa mlinzi wa shule hiyo wengine ni mmiliki wa shule, Edward Shayo maarufu “Kingsize” na mwalimu wa nidhamu wa shuleni hapo, Laban Nabiswa.
Mwanafunzi huyo aliuawa usiku wa Novemba 6, 2017 kwa kupigwa mapanga na Chacha na baadaye akawaita kwa simu Shayo na Nabiswa ambao baada ya kufika, Shayo aliagiza mwili utupwe mtoni.
Akizungumza jana na Mwananchi, wakili aliyekuwa akimtetea Chacha, David Shillatu alisema leo atawasilisha notisi ya kukata rufaa kupinga mambo mawili; hukumu pamoja na adhabu aliyopewa mteja wake.
“Nitawasilisha notisi kesho (leo) kisha nikipewa tu records (kumbukumbu) za Mahakama nitaandaa sababu za rufaa na kuziwasilisha Mahakama ya Rufaa halafu tutasubiri taratibu zingine,” alisema.
Pia Soma
- Lukuvi: TTCL, Tanesco wadaiwa sugu kodi ya ardhi
- Mwanafunzi afanya mtihani dakika 30 baada ya kujifungua
- Rais Pakistan akamatwa kwa rushwa
- Mwanajeshi Uganda auawa kisa 'kiroba' cha pombe
Wakili Patrick Paul aliyemtetea Nabiswa ambaye ni raia wa Kenya, alisema suala la kukata rufaa ni la mteja na bado alikuwa hajapata maelekezo hayo.