Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aliyehukumiwa kunyongwa kwa kumuua aliyeoa mkewe yamkuta tena

Law Photo Aliyehukumiwa kunyongwa kwa kumuua aliyeoa mkewe yamkuta tena

Wed, 30 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MAHAKAMA ya Rufani Tanzania Kanda ya Mtwara imetupilia mbali rufani ya Mahamudu Chupa, aliyehukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kumuua mume mwenzake baada ya kuona haina mashiko.

Hukumu ya Mahakama hiyo ilitolewa na jopo la majaji watatu, Jaji Gerald Ndika, Rehema Kerefu na Penterin Kente baada ya kupitia hoja za kupinga adhabu zilizowasilishwa na mrufani kupitia Wakili Robert Dadaya.

Katika hukumu hiyo, mrufani alitiwa hatiani na Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara kwa kosa la kuua kwa kukusudia na kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa.

Jamhuri katika shauri hilo ilikuwa na mashahidi sita na kwamba mrufani na marehemu Dickson Mnimbo walikuwa wakiishi kijiji kimoja cha Nkowe wilayani Ruangwa mkoani Lindi.

"Hakuna ubishi kwamba marehemu alikuwa akiishi na shahidi wa kwanza, Helena Chitanda baada ya shahidi huyo kuvunja uhusiano wa kimapenzi wa awali kati yake na mrufani," lilisema jopo hilo la majaji.

Inadaiwa kuwa mchana wa Januari Mosi, 2018, mrufani akiwa na rafiki yake aliyetajwa kwa jina la Jirani, walimkuta shahidi wa kwanza akiwa na Mnimbo (marehemu), wakamvamia Mnimbo na kumpiga hadi kusababisha kifo chake.

Inadaiwa kwamba mrufani kufanya kitendo hicho ilikuwa kulipiza kisasi kwa Mnimbo kwa kumchukua aliyekuwa mpenzi wake.

Ripoti ya uchunguzi wa daktari ilionyesha kifo cha Mnimbo kilisababishwa na jeraha kichwani.

Mrufani pamoja na sababu zingine za kupinga adhabu, alidai kwamba jaji hakuchambua vizuri ushahidi wa utetezi na kwamba siku ya tukio, mrufani alifuata vitu vyake kwa shahidi wa kwanza.

Katika utetezi huo, alidai walipigana na Mnimbo na kwamba Jamhuri walishindwa kutoa ushahidi wa kuonyesha jinsi alivyomjeruhi.

Jopo la majaji baada ya kupitia hoja za pande zote mbili, lilisema hakuna ushahidi wa kuonyesha kulikuwa na kupigana kati ya mrufani na Mnimbo.

Mahakama ilikubaliana na hoja za Jamhuri zilizowasilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Ajuaye Zegeli kwamba rufani itupwe haina mashiko na upande wao walikuwa na ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuwa mrufani alitenda tukio hilo.

Jopo la majaji baada ya kusema hayo lilitupilia mbali rufani hiyo kwa sababu haina mashiko kisheria. Mrufani ataendelea kutumikia adhabu aliyopewa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live