Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aliyegonga wanaofanya mazoezi Mwanza kizimbani

Picha Aliyegonga Data Aliyegonga wanaofanya mazoezi Mwanza kizimbani

Wed, 2 Aug 2023 Chanzo: mwanachidigital

Oswald Binamungu (39), mkazi wa Buswelu Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza amefikishwa mahakamani akikabiliwa na shtaka lenye makosa 15 likiwemo la kuendesha gari kwa kasi na kusababisha vifo vya watu sita na kujeruhi wengine tisa.

Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Ileela leo Agosti Mosi, 2023, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Anitha Mweli amedai Oswald alisababisha majeruhi na vifo hivyo kwa wakuendesha kwa uzembe gari aina ya Toyota Hilux Double Cabin.

Amedai katika tukio hilo lililotokea Julai 22, 2023, mshtakiwa huyo aliwagonga kwa nyuma watu waliokuwa wanafanyamazoezi ya kukimbia mchakamchaka katika barabara ya Kiseke wilayani Ilemela.

‘’Akiendesha gari kwa uzembe na mwendokasi, mshtakiwa aliwagonga kwa nyuma waliokuwa wanafanya mazoezi na kusababisha vifo na madhara makubwa kinyume na Kifungu namba 40 (1), 63 (2) (a) na 27 (b) cha Sheria ya Usalama Barabarani namba 168 marejeo ya mwaka 2002,’’ amedai Wakili Mweli

Akisaidiana kusoma hati hiyo na Wakili mwenzake wa Serikali, Mwanahawa Changale, Wakili Mweli amewataja waliofariki katika ajali hiyo kuwa ni Selestine Daudi, Hamis Nehemia, Makongoro Manyanda, Peter Fredrick, Amani Matinde na Shadrack Safari.

Mbele ya Hakimu Mkazi, Amani Sumari, Wakili Mweli amewataja watu tisa waliojeruhiwa katika ajali hiyo kuwa ni Grace Chacha, Remigius Ponsian, Baraka Nehemia, Steven Tweve, Maulid Mashaka, Patrick Mathias, Godfrey Benard, Peter Simikwa na Magnus Masanja.

"Upelelezi wa shtaka hili umekamilika na tunaiomba Mahakama kupanga tarehe kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali ya kesi hiyo," amesema Anitha.

Mshtakiwa anayetetewa na Mawakili Linus Amri na Steven Kitale amekana mashtaka dhidi dhidi yake na kuachiwa kwa dhamana baada ya kukidhi masharti ya kuwa na wadhamini wawili, mmoja akiwa mtumishi wa umma waliosaini hati ya dhamana ya Sh10 milioni kila mmoja.

Hakimu Sumari ameahirisha shauri hilo hadi Agosti 10, 2023 kwa mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali.

Chanzo: mwanachidigital