Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aliyefungwa jela miaka 30 kwa unyang’anyi aachiwa huru

Mahakamaaaaaaa Aliyefungwa jela miaka 30 kwa unyang’anyi aachiwa huru

Thu, 24 Nov 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama ya Rufaa Dar es Salaam, imemwachia huru Abdulaziz Omary, aliyekuwa amehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.

Omary alikata rufaa hiyo kupinga kutiwa hatiani na adhabu ya kifungo cha miaka 30 aliyopewa katika Mahakama ya Wilaya Kinondoni.

Katika rufani hiyo, Omary alikuwa na hoja saba ikiwemo kwamba, upande wa mashitaka ulishindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yake na pia mnyororo wa ulinzi wa vitu vinavyodaiwa kuibwa haukuwa sahihi.

Uamuzi huo ulitolewa chini ya jopo la majaji watatu, Jaji Ferdinand Wambali, Winfrida Korosso na Sam Rumanyika.

Katika uamuzi huo, pamoja na mambo mengine, majaji hao walikubaliana na hoja za mrufani kwamba upande wa mashitaka ulishindwa kuthibitisha mashitaka dhidi ya mrufani pasipo kuacha shaka yoyote.

Katika hoja saba za mrufani, mahakama ilitupilia mbali hoja ya kwanza na kukubaliana na hoja sita zilizobaki.

“Kutokana na hali hiyo, rufaa hiyo imefanikiwa tunatengua hatia na adhabu, tunaamuru mrufani aachiwe huru mara moja labda kama kutakuwa na sababu zingine za kisheria zitakazofanya aendelee kubaki gerezani,” alisema.

Katika kesi hiyo, ilidaiwa kwamba Aprili 12, 2017 eneo la Kimara, Dar es Salaam, mrufani aliiba vifaa mbalimbali vya gari aina ya Toyota Verossa vyenye thamani ya Sh milioni 1.7, mali ya Salmin Mfinaga.

Ilidaiwa kwamba mrufani alitumia bisibisi kujipatia mali hizo ambapo alimsababishia majeraha upande wa juu wa kushoto wa jichoni.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live