Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aliyedaiwa kusafirisha dawa za kulevya aachiwa

51414 Pic+mtuhumiwa

Wed, 10 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemwachia huru mfanyabiashara, Kihemba Mchungu, aliyekuwa anakabiliwa na kesi ya  kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa gramu 81.8

Mshtakiwa huyo ameachiwa jana Jumatatu Aprili 8, 2019 na hakimu Maira Kasonde baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha ushahidi pasi na shaka.

Hakimu Kasonde amedai upande wa mashtaka ulileta mashahidi sita na vielelezo mbalimbali na upande wa utetezi ulikuwa na mashahidi wawili.

Amesema miongoni mwa mashahidi hao ni ofisa wa polisi kutoka kitengo cha dawa za kulevya aliyemtaja kwa jina la moja la Rwamba, ambaye  anadaiwa kukamata dawa hizo wakati wa upekuzi katika nyumba ya mshtakiwa iliyopo Magomeni.

Hata hivyo, upande wa utetezi ulionyesha mashaka ya upatikanaji dawa hizo kutokana na mashahidi wake akiwamo mwenyekiti wa serikali ya mtaa anakoishi mshtakiwa, Sharifa Mrisho.

Hakimu Kasonda amesema kwa mujibu wa shahidi huru aliieleza  Mahakama kwamba alipofika nyumbani kwa mshtakiwa alikuta tayari maofisa wa polisi kitengo cha dawa za kulevya wameshaingia ndani kufanya upekuzi, huku mshtakiwa akiwa nje amefungwa pingu.

Ameendelea kudai Sharifa akiwa na mshtakiwa waliingia ndani na  kufahamishwa kuwa walikuwa wanatafuta dawa za kulevya.

Hakimu ameeleza kuwa shahidi huyo hakuitambua hati ya upekuzi wala mfuko uliokuwa na pakiti mbili za dawa za kulevya ambazo zilizotolewa mahakamani.

"Nadhani ushahidi wa upande wa mashtaka  una upungufu ulihitaji kuungwa mkono, ushahidi wa upande wa utetezi unatikisa ushahidi wa upande wa mashtaka katika kesi hii sikuelewa kwa nini upande wa mashtaka haukuleta mashahidi muhimu kama Hussein Salum na Sharifa, ambao walikuwa viongozi wa serikali ya mtaa eneo hilo," amehoji hakimu Kasonde.

Amesema ushahidi huo unaonyesha kuna mashaka ya uwapo wa kielelezo hicho kilichopatikana kwenye nyumba kwani kuna uwezekano kikawa kimepandikizwa.

Amesema kutokana na hali hiyo, Mahakama inamuona mshtakiwa hana hatia na inamuachia chini ya kifungu 235 cha mwenendo wa makosa ya jinai.



Chanzo: mwananchi.co.tz