Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aliyedaiwa kuomba rushwa ya Sh200 milioni bado anajadiliana na DPP

Aliyedaiwa kuomba rushwa ya Sh200 milioni bado anajadiliana na DPP

Fri, 29 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Aliyekuwa mchunguzi mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini Tanzania (Takukuru), Cosmas Batanyita amedai bado yupo katika mazungumzo na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).

Mshtakiwa huyo ameeleza hayo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Ijumaa Novemba 29, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustina Mmbando wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Batanyita anakabiliwa na mashtaka saba likiwemo la kuomba rushwa ya Sh200 milioni na kutakatisha fedha.

Batanyita baada ya kueleza hayo, wakili wa Serikali mwandamizi, Wankyo Simon amedai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na hakimu anayeendesha kesi hiyo yupo nje ya Mkoa kikazi.

"Upelelezi wa kesi hii bado haujakamilika na hakimu anayesikiliza kesi hii Yupo nje ya mkoa kikazi, tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa," amedai Simon.

Novemba Mosi, 2019 mshtakiwa huyo aliieleza mahakama hiyo kuwa ameandikia barua ya kukiri na kuomba msamaha kwa DPP.

Hakimu Mmbando baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote, ameahirisha kesi hiyo hadi Desemba 13, 2019 itakapotajwa tena.

Mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na mashtaka ya kutakatisha fedha yanayomkabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.

Alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Agosti 9, 2019 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 76/2019.

Kati ya mashtaka hayo saba, mashtaka matatu ni ya kushawishi rushwa, moja la kuomba na kupokea rushwa na mashtaka matatu ni ya kutakatisha fedha.

Katika kesi ya msingi, Batanyita akiwa mwajiriwa wa Takukuru anadaiwa Februari 9, 2019 katika eneo la Upanga, Dar es Salaam alishawishi na kuomba rushwa  ya Sh200 milioni kutoka kwa Hussein Gulamal Hasham ili aweze kuharibu ushahidi katika kesi ya ukwepaji wa kodi ilivyokuwa inamkabili Hussein, wakati akijua  kuwa upelelezi wa kesi hiyo ulikuwa unaendelea katika Ofisi ya Takukuru.

Pia, anadaiwa Februari 10, 2019 katika eneo la Sabasaba, Batanyita alijipatia dola  20,000 za Marekani kutoka Faizal  Hasham ikiwa ni ahadi ya kuharibu ushahidi katika kesi ya ukwepaji kodi inayomkabili Hasham, wakati akijua upelelezi wa kesi hiyo ulikuwa unaendelea.

Chanzo: mwananchi.co.tz