Siha. Mahakama ya Wilaya ya Siha mkoani Kilimanajaro, imemhukumu Goodluck Lazaro (23) maarufu babuu mkazi wa kijiji cha Merali kutumikia kifungo cha 30 jela kwa kosa la ubakaji.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na hakimu Jasmine Abdul baada ya kuridhika na ushahidi wa mashahidi watano akiwamo daktari, mwanamke aliyebakwa na mwenyekiti wa kijiji hicho.
Hakimu Jasmine alisema ushahidi huo haukuacha shaka ndani yake na Mahakama imemtia hatiani kwa kosa hilo.
Awali, mwendesha mashtaka wa Serikali, Simon Feo alidai kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Agosti 4 saa 10:00 jioni kijijini hapo kwa baada ya kutoroka gereza la Karanga Moshi.
Feo alidai mshtakiwa wakati anarudi kijiji kwao akiwa njiani alikutana na mwanamke na kumkamata kwa nguvu kisha kumburuza kwenye Pori la Kwanduli na kumuingilia bila ridhaa yake.
Aliendelea kuwa mshtakiwa alihukumiwa kifungo cha miezi sita kwa kosa la wizi kesi namba 164/ 2018 na Mahakama ya Mwanzo Sanya juu Aprili 4 na ilitegemewa kumaliza kifungo chake Agosti 7, lakini siku tatu kabla ya kumaliza kifungo alipotoroka gerezani. Huyo mshtakiwa alibakiza siku chache kumaliza kifugo chake lakini akatoroka gerezani alipokuwa anarudi kijijini kwao akakutana na huyo mwanamke na kumbaka.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mwendesha mashtaka aliomba Mahakama kutoa adhabu kali dhidi ya mshtakiwa kutokana na usugu wake na amefikia hatua ya kutoroka kifungoni.