Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aliyebaka ajuza wa miaka 92 kupata utajiri kunyongwa

Hukumu Pc Data Aliyebaka ajuza wa miaka 92 kupata utajiri kunyongwa

Wed, 24 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

m.Mkazi wa Kijiji cha Gocho, wilayani Hanang’, Mkoa wa Manyara, Edmund Emmanuel, atanyongwa hadi kufa baada kutiwa hatiani kwa kosa la kumbaka ajuza wa miaka 94 na kumsababishia kifo, akiamini kitendo hicho kitampa utajiri.

Mkazi huyo anayejulikana pia kwa jina la Edmund Mchuno, alikiri kuwa ugumu wa maisha, ulimfanya aende kwa mganga wa kienyeji, aliyemshauri afanye mapenzi na mwanamke mzee aliyepooza ili apate utajiri.

Kesi yake ni ushahidi juu ya ushahidi wa jinsi waganga wa kienyeji wanavyochangia kukuza imani za kishirikina, ambazo zimegharimu maisha ya watu wengi na kuacha familia nyingi katika ugomvi na kutoelewana.

Bibi kizee huyo wa miaka 92 (jina tunalo), alibakwa jioni ya Juni 13, 2020 akiwa amelala ndani ya nyumba yake. Alifariki saa chache baadaye kwa shambulio la moyo. Hakuwa na uwezo wa kutembea na aliishi na ugonjwa wa kupooza kwa miaka mingi.

Isingekuwa mmoja wa wajukuu wa bibi huyo, Reuben Jeremiah kusikia sauti ya bibi yake akiomba msaada na kwenda eneo la tukio, pengine Edmund angekwepa mkono wa sheria.

Jeremiah alikimbia kuelekea eneo la tukio na kumkuta bibi yake akiugulia maumivu makali. Bibi huyo alimweleza alikuwa amevamiwa na kijana mhuni.

Akiwa bado amesimama mlangoni mwa nyumba ya bibi huyo, ghafla Edmund alitoka ndani ya chumba hicho na kumsukuma na kukimbilia nje.

Baada ya kufanikiwa kutoka nje, Edmund aliamua kuufunga kwa nje mlango wa chumba alichokuwemo Jeremiah ili kumzuia asitoke na kumfuatilia.

Akiwa bado anafikiri cha kufanya, Jeremiah alichungulia nje kwa kutumia tundu la dirisha na kumwona dada aitwaye Rehema na kumwomba amfungulie mlango.

Rehema alipofungua mlango alishuhudia bibi yule akiwa katika maumivu, hivyo alikwenda kuita watu akimwacha Jeremiah akilinda nyumba ile hadi watu wengine walipofika kutoa msaada.

Hali ya ajuza huyo ilizidi kubadilika na kuwa mbaya kadiri muda ulivyozidi kwenda kabla ya kufikwa na mauti saa 5 usiku.

Taarifa za kubakwa kwa bibi huyo zilisambaa kama moto ulioshika nyasi kavu hadi kumfikia Mwenyekiti wa Kitongoji, Scandrian Patrice, aliyekwenda eneo la tukio na kumkuta bibi huyo akiwa hai lakini kwenye maumivu makali.

Mwenyekiti huyo aliamuru mgambo wa kitongoji chake kumsaka na kumkamata Edmund. Edmund alikamatwa majira ya saa 6 usiku akiwa nyumbani kwake.

Baada ya polisi kufika kwenye ofisi ya kijiji ambapo Edmund alikuwa akishikiliwa, Mtendaji wa Kijiji hicho, Alphonse Francis alifungua mlango alipohifadhiwa Edmund na kumuuliza sababu ya kufanya unyama ule.

“Mshitakiwa alinieleza alifanya kosa hilo kutokana na ugumu wa maisha. Alinieleza alikwenda kwa mganga wa kienyeji aliyemwambia afanye mapenzi na mwanamke mzee aliyepooza kama sharti la kupata utajiri,” alisema Francis wakati akitoa ushahidi katika Mahakama Kuu, masjala ndogo ya Arusha, Babati.

Daktari Erasto Mushi aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu, aliiambia Mahakama kuwa aligundua mikwaruzo kwenye shingo, mgongo na sehemu kadhaa za mwili wa marehemu.

Pia alichunguza sehemu za siri za marehemu na kuzikuta zikiwa wazi na maji maji meupe ambazo aliiambia mahakama zilikuwa ni mbegu za kiume.

Kwa kuzingatia umri wake na majeraha aliyokuwa amepata, alisema Dk Mushi, kifo cha bibi huyo kilitokana na shambulio la moyo alilopata kutokana na purukushani ya kubakwa.

Edmund ajitetea

Katika utetezi wake, Edmund alidai hakuwa eneo la tukio wakati kitendo hicho kikitokea. Alidai siku ya tukio saa 7:30 mchana alipanda basi la Mtei kutoka Dodoma kuelekea Katesh kupitia Singida na kufika Katesh saa 12 jioni.

Alidai saa 12:50 alichukua usafiri mwingine kutoka Katesh hadi Gitting ambapo alifika saa tatu usiku.

“Nilichukua usafiri wa pikipiki kutoka Gitting hadi Gocho B nainapoishi. Baada ya kufika nyumbani sikwenda popote,” alisema huku akionesha tiketi za basi kuthibitisha madai yake.

Edmund pia alikana kumbaka ajuza huyo, akidai kuwa Jeremiah alitunga ushahidi dhidi yake, kwa kuwa hawakuwa wakielewana.

Alieleza kuwa Jeremiah aliwahi kulisha kundi la ng’ombe wake kwenye majani yake na miezi miwili kabla ya tukio alipeleka malalamiko kwenye ofisi ya kijiji aliyodai ilimuonya Jeremiah. “Kuanzia pale uhusiano wetu ulizidi kuwa mbaya na kila tulipokutana Jeremiah alinitukana,” alidai.

Wakati wa usikilizwaji wa kesi dhidi yake, Edmund hakuwahi kupinga madai kuwa bibi yule alibakwa, ila alisisitiza yeye hakuwepo eneo la tukio wakati kosa hilo likitendeka.

Jaji akubaliana na daktari

Jaji John Kahyoza alikubaliana kwa kiasi kikubwa na maelezo ya daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa bibi huyo.

“Sipati sababu ya kutokubaliana na maelezo ya kitaalamu ya daktari kuhusu sababu ya kifo cha (anataja jina). Hakuna ushahidi wa kudhoofisha ushahidi wake. Ninaona kuwa imethibitishwa kuwa marehemu alikuwa mzee sana, mgonjwa, amepooza na kwamba alibakwa, kwa mujibu wa ushahidi wa Dk Erasto Mushi.

“Kumweka mwanamke wa umri ule katika purukushani na msongo uliosababishwa kitendo cha kujamiiana kwa nguvu lazima kumletee mshtuko. Ni jambo ambalo hakutegemea katika umri ule, na ukizingatia umri wake, si jambo la ajabu kuwa alipata shambulio la moyo,” alisema Jaji Kahyoza.

Nani aliyebaka?

Baada ya kukubaliana na ushahidi wa daktari kuwa kubakwa ndiko kulimsababishia ajuza yule kifo, Jaji Kahyoza aliendelea kuchambua ushahidi ili kujiridhisha kama ni Edmund ndiye aliyebaka au la.

Kifungu cha 203 cha Kanuni ya Adhabu kimeeleza mazingira ambayo mtu huchukuliwa kuwa amesababisha kifo cha mtu mwingine, ingawa kitendo alichofanya kinaweza kisiwe sababu ya papo hapo au sababu pekee ya kifo hicho.

Kwanza, endapo mtu atakuwa amemsababishia mtu mwingine majeraha ambayo yanaweza kusababisha upasuaji au matibabu mengine ambayo husababisha kifo.

Pili, mtu atachukuliwa kusababisha kifo pale kitendo cha kufanya au kutofanya jamba analopaswa kufanya kitaharakisha kifo cha mtu anayesumbuka na ugonjwa wowote au jeraha.

“Hakuna shaka kuwa marehemu alikuwa mtu wa kitandani, mzee na mgonjwa wa kupooza. Mtu aliyembaka, kwa mujibu wa daktari, aliharakisha kifo chake. Alimsababishia shambulio la moyo. Hivyo, nasema kwamba mtu aliyembaka ndiye aliyesababisha kifo chake,” alisema Jaji Kahyoza.

Aomba kupunguziwa adhabu

Baada ya kuwa ametiwa hatiani kwa kosa la kuua ambalo adhabu yake pekee ni kunyongwa hadi kufa, wakili wa Edmund aliomba mahakama impunguzie adhabu mteja wake akieleza kuwa bado ni kijana mdogo na kwamba hiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kutenda kosa hilo.

Pia aliiomba mahakama izingatie ukweli kuwa tayari mteja wake alikuwa amekaa mahabusu kwa miaka mitatu.

“Alifanya kosa hilo (kuua) wakati akimbaka marahemu. Alidanganywa kuwa kama atambaka mwanamke mzee aliyepooza atakuwa tajiri, na si vinginevyo. Anajutia na anaomba unafuu wa adhabu,” alisema wakili Chami.

Maombi hayo hayakufanikiwa kuishawishi Mahakama kutoa adhabu kinyume na ile iliyotamkwa katika kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu, yaani kunyongwa hadi kufa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live