Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aliyeachiwa kwa mauaji ahukumiwa kunyongwa

Cybercrime 1140x640 Aliyeachiwa kwa mauaji ahukumiwa kunyongwa

Sat, 17 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama ya Rufani imebatilisha hukumu iliyomwachia huru, Jilala Jihusa na kumhukumu adhabu ya kifo baada ya mahakama kuikubali rufaa iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) mwaka 2021.

Agosti 29, 2021 Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya ilimwachia huru Jihusa, mkazi wa Kijiji cha Kapunga wilayani Mbarali aliyekuwa ameshtakiwa kwa mauaji ya kukusudia ya Mbuga Masanja, yaliyotokea Agosti 4, 2016.

Jaji Dunstan Ndunguru alimwachia huru kwa maelezo upande wa mashtaka ulikuwa umeshindwa kuthibitisha shtaka la mauaji na kwamba maelezo ya kukiri kosa ya mshtakiwa hayakutolewa kwa hiyari, bali alilazimishwa tu kuyatia saini.

DPP hakuridhika na hukumu hiyo akakata rufaa Mahakama ya Rufani Tanzania, ambayo baada ya kusikiliza rufaa ilitoa hukumu Februari 14, 2024 na kubatilisha hukumu ya awali, ikisisitiza shtaka hilo lilithibitishwa.

Jopo la majaji watatu, Dk Gerald Ndika, Sam Rumanyika na Zainab Muruke limesema limeridhika kuwa maelezo ya mshtakiwa ya kukiri kosa aliyoyatoa Polisi na kwa mlinzi wa amani yaliyokataliwa na mahakama, yaliungwa mkono na ushahidi wingine.

Pia majaji hao walisema sababu iliyotolewa na mahakama kuwa ushahidi wa mmoja wa mashahidi wa Jamhuri kuhusu lini alikamatwa ulikuwa wa kujichanganya si sawa, kwani kumbukumbu zinaonyesha alikiri kukamatwa Oktoba 28, 2016.

“Tunaona kesi ya upande wa mashtaka ilithibitishwa pasipo kuacha shaka. Sababu tano za rufaa za DPP zinakubaliwa. Tunabatilisha uamuzi wa Mahakama Kuu na kuibadilisha hukumu ya kuachiwa huru kuwa ya kunyongwa hadi kufa,” imesema sehemu ya hukumu.

Mauaji yalivyofanyika

Siku ya tukio, mdogo wa marehemu aliwaona kaka yake na mshtakiwa wakiwa ndani ya nyumba,  mshtakiwa alikuwa na mpango wa kununua ng’ombe watatu wa Masanja kwa Sh1.65 milioni na angemlipa watakapofika eneo la Chimala.

Hata hivyo, tangu siku hiyo Masanja hakuonekana tena hadi Agosti 10, 2016 mwili wake ulipopatikana ukiwa umetupwa katika msitu wa Kapunga na taarifa za kupotea kwake zilikuwa zimeripotiwa polisi. Mtu wa mwisho kuwa naye ni Jihusa.

Jihusa alikamatwa na kushtakiwa kwa mauaji ya Masanja na upande wa mashtaka uliegemea zaidi ushahidi kuwa mshtakiwa ndiye mtu wa mwisho kuwa naye kabla ya kifo chake na pia uliegemea maelezo yake ya kukiri kosa la mauaji.

Katika utetezi, alikanusha kuhusika na mauaji hayo na kueleza kuwa siku ya tukio hakuwepo kijijini yeye pamoja na wazazi wake, kwani walikuwa wameenda kwenye harusi.

Aliyakataa maelezo yake ya kukiri kosa akisema yalipatikana baada ya kuteswa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live