Dar es Salaam. Mmoja wa washtakiwa wa kesi za uhujumu uchumi aliyeachiwa kwa utaratibu wa majadiliano kati yake na ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka nchini (DPP), amekamatwa akidaiwa kufanya utapeli.
Mtuhumiwa huyo anadaiwa kuchukua fedha kwa watu na kuwaambia kuwa anawapelekea maofisa wa ofisi ya DPP rushwa ili wawasaidie ndugu zao watoke mapema kwa utaratibu wa majadiliano.
Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, Biswalo Mganga amemtaja mtuhumiwa huyo ( jina limehifadhiwa) leo Alhamisi Machi 12, 2020 katika mkutano wake na waandishi wa habari, kwamba mtu huyo amekuwa akifanya vitendo hivyo katika maeneo mbalimbali.
"Anapofanya hivi inaonekana watumishi wa DPP na maofisa wa Serikali wanajiingiza katika rushwa. Alipofika tulimgundua na kutoa taarifa polisi na kumkamata, alikuwa amechukua Sh1.2 milioni kwa Edward Mtalima na baadhi ya watu wengine."
"Amechukua fedha hizi kwa madai anataka kumsaidia Mtalima ambaye ni mshtakiwa katika kesi namba saba ya uhujumu uchumi ya mwaka 2019. Hatuwezi kuvumilia upumbavu wa namna hii na atafikishwa mahakamani leo akikabiliwa na mashtaka matatu," amesema Mganga.
Mganga amesema tayari ameshawapa maelekezo mawakili na hati ya mashtaka dhidi yake imeshaandaliwa na atasomewa leo huku akitoa onyo kwa wananchi wengine kutoingia katika vitendo hivyo na watakaobainika hatosita kuwachukulia hatua.
Pia Soma
- Trump azuia raia wa Ulaya kuingia Marekani
- Corona yatangazwa kuwa janga la kimataifa
- Chadema wasema bado Sh90 milioni kuwatoa jela viongozi wote
"Wengine wanakuja ofisini kwa kigezo cha kuulizia kesi za ndugu zao wakiambatana na watu wanaowaacha chini. Wanawaambia kwa DPP huwezi kuingia, mimi nitaingia peke yangu, wakitoka wanawaambia tumeshamalizana na DPP ndiyo maana huyu tulimuwekea mtego," amesema Mganga.