Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Alikwenda mazoezi hakurudi hadi sasa

47427 PIC+MAZOEZINI

Wed, 20 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkazi wa kijiji cha Mwandege wilayani Mkuranga amepotea kwa zaidi ya wiki moja sasa baada ya kwenda mazoezini asubuhi. Ramadhan Wihanji (38), aliondoka nyumbani kwake kitongoji cha Chatembo Jumatatu Machi 11 asubuhi, hakurudi tena hali iliyoacha simanzi kwa familia yake inayoendelea kumtafuta.

Kwa mujibu wa maelezo ya mke wake, Sofia Mbonde, Ramadhan (pichani) alikuwa na kawaida akitoka msikitini asubuhi kufanya mazoezi ya kuendesha baiskeli akipita maeneo ya Kigamboni, Mbagala, Vikindu hadi Mkuranga.

“Aliondoka hapa nyumbani saa 12:00 asubuhi na baiskeli yake ila hatuna uhakika kama alielekea njia ya Mkuranga upande wa Kigamboni au Mbagala. Kawaida huwa anarudi saa mbili hivi kisha anajiandaa kuelekea kazini Kariakoo. Ilipofika saa tano nilimtafuta kwenye simu haikupatikana na nikapiga kazini kwake kuulizia hakuwa amefika. Baadaye nikatoa taarifa kwa ndugu tukaanza kumtafuta maeneo mbalimbali.

“Tumetoa taarifa kituo cha polisi Maturubai (Mbagala Kizuiani) pia tumetembelea vituo vya Mkuranga, Chang’ombe, Kilwa Road, Oysterbay hadi Central (kituo kikuu). Pia, tumemtafuta hospitali mbalimbali na kote huko hatujampata wala taarifa zake. Mungu atusaidie,” alisema Sofia aliyekuwa amempakata mtoto wake wa mwezi mmoja huku ndugu na majirani wakiwapo kumfariji.

Kamanda wa polisi mkoa wa Temeke, Amon Kakwale, aliliambia Mwananchi kuwa hana taarifa lakini akasihi ndugu waendelee kutembelea vituo vya polisi na hospitali.

“Mwandege ipo wilaya nyingine lakini kwa kuwa wametoa taarifa Mbagala basi tutaendelea kuwapa ushirikiano kadri watakavyokuwa wanakuja,” alisema.

Naye kamanda wa polisi Kanda Maalumu ya Kibiti, Onesmo Lyanga alipoulizwa alijibu kwa kifupi: “Kwa kuwa ndugu wametoa taarifa polisi, tutalifanyia kazi suala hili.” Nakushukuru ndugu mwandishi kwa kunipa taarifa pia.”



Chanzo: mwananchi.co.tz