Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Alichokisema mtumishi wa Tanesco kesi ya Gugai

73183 Gugai+pi

Tue, 27 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Emillian Richard, fundi mchundo  wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu  jinsi alivyokwenda nyumbani kwa aliyekuwa mhasibu mkuu wa Takukuru, Godfrey Gugai baada ya kupata malalamiko kutoka kwa mshtakiwa huyo.

Richard, shahidi wa 24  katika kesi ya utakatishaji fedha na kumiliki mali zilizozidi kipato inayomkabili Gugai na wenzake watatu, ameeleza hayo leo Jumanne Agosti 27, 2019 wakati akitoa ushahidi katika kesi hiyo.

Akiongozwa na wakili wa Serikali mwandamizi, Awamu Mbagwa akisaidiana na Ipyana Mwakatobe na Estazia Wilson, amedai alimfahamu Gugai baada ya kufika katika ofisi za Tanesco  kutoa malalamiko kuwa umeme ni mdogo katika nyumba yake.

"Nilimfahamu mshtakiwa baada ya kuja katika ofisi za Tanesco zilizopo Tegeta na kudai kuwa umeme ni mdogo katika nyumba yake hivyo anaomba kwenda kuangaliziwa,” amedai Richard.

Shahidi huyo amedai kabla ya kuhamishiwa kituo cha  Makumbusho mwaka 2016, alikuwa msimamizi wa kituo cha Tanesco Tegeta kuanzia mwaka 2013.

Mbele ya hakimu mkazi mkuu, Thomas Simba, shahidi huyo amedai mbali na Gugai kwenda kutoa malalamiko, alikwenda kuomba afungiwe umeme  katika nyumba  yake mpya.

Habari zinazohusiana na hii

"Baada ya kupata malalamiko hayo meneja wangu  alinituma niende  nyumbani kwake (Gugai)  kufanya ukaguzi, hivyo tuliongozana na Gugai hadi nyumbani kwake Boko Ununio,” amesema Richard.

Amedai baada ya kufika nyumbani kwa Gugai, alikuta umeme mdogo, “Baada ya hapo tulimfungia umeme mwingine katika nyumba yake mpya na  alijaza fomu nne katika mchoro na akasaini.”

Fomu hizo zilipokelewa mahakamani hapo kama kielelezo.

Baada ya kusikiliza ushahidi huo, hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi kesho.

Tayari mashahidi 24 wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi wao dhidi ya Gugai.

Miongoni mwa mashahidi hao ni Amina Kilemba (81) aliyeieleza mahakama hiyo kuwa yeye ndio aliyemuuzia Gugai kiwanja namba 64 kilichopo  Boko Ununio kwa Sh80 milioni.

Kilemba amedai kiwanja hicho kilikuwa ni cha mwanae Mize Kilemba (marehemu).

Mbali na Gugai, washitakiwa wengine katika kesi hiyo  ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasin Katera.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na makosa 43, kati ya hayo 19 ni ya kughushi, 23 ni utakatishaji fedha na moja ni kumiliki mali zilizozidi kipato halali linalomkabili  Gugai.

Gugai anakabiliwa na kosa la kumiliki mali kinyume na kipato chake, akidaiwa kutenda  kosa hilo kati ya Januari 2005 na Desemba 2015.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz