Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Akutwa kajinyonga jirani na nyumba ya mkewe

Kifo Mautii Akutwa kajinyonga jirani na nyumba ya mkewe

Mon, 19 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jeshi la Polisi mkoani Mtwara linafanya uchunguzi wa tukio la mwanaume mmoja kujinyonga katika kijiji cha Majengo kata ya Ziwani Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara.

Mwanaume huyo amekutwa amejinyonga jirani ya nyumba ya mkewe ambaye walikorofishana.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Jumatatu Februari 19,2024, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, ACP-Mtaki Kurwijila amesema mwili ulikutwa jana Jumapili Februari 18, 2024 saa 12 asubuhi ukining’inia kwenye mti wa mkorosho.

Amesema kwa mujibu wa mkewe, mumewe alitoka nyumbani kwake Februari 12 na kwenda kusikojulikana baada ya kutoelewana.

Hata hivyo, kaimu kamanda huyo amesema mwili wake ulikutwa umefungwa mtandio shingoni ukiwa unaning’inia kwenye tawi la mkorosho na sababu za kujinyonga ni wivu wa mapenzi.

Kamanda Kurwijila amedai mume huyo anamtuhumu mkewe kuwa na uhusiano na mwanume mwingine kwa mujibu wa ujumbe wa maandishi uliokutwa kwenye karatasi aliyoiacha.

Amesema mwili wa mwanaume huyo kwa sasa umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara Ligula, kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

“Marehemu alitoweka nyumbani baada ya kumtuhumu mkewe kuwa na mwanaume mwingine nje ya ndoa yao na tangu Februari 12 alihama nyumbani hadi alipoonekana akiwa amejinyonga jirani na nyumba ya mkewe,” amesema ACP Kurwijila.

Mke asimulia

Akizungumza na Mwananchi digital, mke wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Fatuma Ally amesema siku ya tukio aliwahi kwenda shambani.

Lakini baadaye alifuatwa na majirani ambao walimpatia taarifa ya mumewe kujinyonga jirani na nyumbani kwake.

“Siku ya tukio niliamka asubuhi nikawahi shambani, nikiwa huko nikafuatwa na majirani zangu kuja kunipa taarifa hii. Nikaambiwa mume wangu amejinyonga kwenye mti wa mkorosho ambao upo nyuma ya nyumba yangu, nilirejea haraka nyumbani na ndoa yetu ina miezi sita tu,” amesema Fatuma na kuongeza;

“Mimi sijui chanzo cha kujinyonga, tangu Jumatatu (Februari 12) aliondoka humu ndani na alibeba kila kitu chake baada ya kukwaruzana, hakunipa talaka na alirudi kwake kijiji kingine, huko ana nyumba yake na hapa ni nyumbani kwangu,” amesema Fatuma.

Akizungumzia hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Majengo, Mohamed Kikulacho amesema tukio hilo limewashangaza kwa kuwa mzee huyo hakuwa na tatizo.

“Kiukweli huyu mzee hakuwa na tatizo lolote ni vema ukiwa na tatizo ukashirikisha watu ili kuweza kupata utatuzi wa tukio linalokusumbua kuliko kufanya hiki cha kujichukua maamuzi ya kunywa sumu ama kujinyonga sio suluhisho la matatizo, ” amesema Kikulacho.

Naye Said Kipande, mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa Msikiti wa Majengo ambaye alikuwa akishirikiana na marehemu kujenga msikiti huo amesema, marehemu alikuwa mtu wa dini hali ambayo ilichangia achaguliwe na waumini wenzake.

“Unajua marehemu alikuwa kiongozi mwenzangu kwenye msikiti wetu, mimi nilikuwa mwenyekiti, inasikitisha hatujajua sababu ya yeye kujinyonga hii kwetu inaleta utata na kuzua hofu kwa jamii yetu,” amesema Kipande.

Mkazi wa Ziwani, Zahara Abdulahman amesema matukio ya kujiua yamekuwa mengi hivi sasa na hawajui sababu hasa ni kitu gani.

Zahara anasema wameendelea kushuhudia watu wakinywa sumu na kufa na wengine hunusurika lakini pia ya kujinyonga yanaendekea kutokea kila wakati.

“Yaani huku vifo vya kujinyonga na kunywa sumu vimekuwa vingi katika kijiji chetu, hii inatutushia amani, sio watoto sio wazee hii inatufanya tuwaze sana na tujiulize kwa nini,” amesema Zahara.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live