Mshtakiwa Peter Lameck (25) anayekabiliwa na kesi ya mauaji ya shangazi aitwaye Isanziye Mwinula (67), amekiri kutenda kosa hilo, lakini akadai kuwa alimuua shangazi yake huyo bila kukusudia, kutokana na tuhuma za kuwaua ndugu zake pamoja na mtoto wake (mshtakiwa), kwa uchawi.
Mshtakiwa huyo amekiri kutenda kosa hilo juzi, Mei 6, 2024, wakati kesi hiyo ilipoigwa kwa ajili ya kuanza kusikilizwa, baada ya kusomewa shtaka linalomkabili.
Hata hivyo, upande wa mashtaka katika kesi hiyo umepinga maelezo hayo ya mshtakiwa huyo, kuwa aliua bila kukusidia, badala yake umedai kuwa aliua kwa kukusudia.
Kufuatia msimamo huo wa upande wa Jamhuri kudai mshtakiwa aliua kwa kukusudia Jaji anayesikiliza kesi hiyo namba 78 ya mwaka 2022, Griffin Mwakapeje aliutaka upande wa mashtaka kuita mashahidi.
Mshtakiwa huyo anadaiwa kumuua Isanzye Mwinula katika tukio analodaiwa kulifanya Machi 22,2021 katika kitongoji cha Zanzibar kijiji cha Wina Wilayani Chato Mkoani Geita kinyume na vifungu vya 196 na 197 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.