Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Akina Mbowe watetewa na mashahidi 15 kati ya 200, Mdee na Bulaya waonywa

93019 Pic+mbowe Akina Mbowe watetewa na mashahidi 15 kati ya 200, Mdee na Bulaya waonywa

Fri, 24 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Upande wa utetezi katika kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi tisa wa Chadema leo Ijumaa Januari 24, 2020 umefunga ushahidi baada ya kuwaleta mahakamani mashahidi 15 badala ya 200 walioahidi.

Sasa kinachosubiriwa ni majumuisho ya kesi hiyo yatakayowasilishwa na upande wa utetezi na ule wa mashtaka Februari 24, 2020 siku ambayo itapangwa tarehe ya hukumu ya kesi hiyo.

Washtakiwa hao kupitia kwa wakili wao Peter Kibatala leo Ijumaa Januari 24, 2020 wamesema hawakusudii kuita mashahidi wengine kwa maelezo kuwa ushahidi uliotolewa unajitosheleza.

Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Thomas Simba baada ya kusikiliza maelezo hayo aliwaonya washtakiwa, Halima Mdee (Kawe) na Ester Bulaya (Bunda)  kwa kukiuka masharti ya dhamana yao baada ya kutoka nje ya Tanzania bila kibali cha mahakama.

Hakimu Simba amesema upande wa mashtaka ulithibitisha kuwa Mdee na Bulaya walikiuka masharti ya dhamana zao.

Amesema barua ya daktari wa Hospitali ya Aga Khan iliyowasilishwa mahakamani hapo na washtakiwa hao aina maana kwenye mkataba wa dhamana yao.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
"Sijaona kama ni busara kuwafutia dhamana washtakiwa hawa wala kuwaambia wadhamini walipe fungu la dhamana waliyosaini, mahakama inawaonya  wote na pia haitashikilia hati zao za kusafiria," amesema Hakimu Simba.

Hakimu huyo ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 24, 2020 siku ambayo pande zote mbili zitawasilisha majumuisho yao kabla kupangwa tarehe ya hukumu.

Kwa pamoja washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 13 yakiwemo ya uchochezi wanayodaiwa kuyatenda Februari 16, 2018 katika viwanja vya Buibui Mwananyamala.

Mbali na Bulaya na Mdee, washtakiwa wengine ni mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe; katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika; naibu katibu mkuu-Zanzibar, Salum Mwalimu na Dk Vicent Mashinji.

Wengine ni Esther Matiko(Tarime Mjini); John Heche (Tarime Vijijini) na Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini).

 

Alichokisema shahidi wa 13

Leo mwanafunzi wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Lumola Kahumbi ameieleza mahakama hiyo jinsi polisi walivyochukua fedha zake na kumlazimisha kuimba wimbo wenye maneno Dola si lelemama.

Lumola, shahidi wa 13 katika kesi ya hiyo ya jinai namba 112/2018 ameeleza hayo wakati akitoa ushahidi mbele ya hakimu Simba.

Katika kesi hiyo mawakili wa upande wa utetezi Peter Kibatala, Profesa Abdallah Safari na upande wa mashtaka wanaongozwa na wakili wa serikali mkuu, Faraja Nchimbi.

Akiongozwa na Kibatala, shahidi huyo amesema katika kituo cha daladala cha Kinondoni Studio wakati akielekea kwa shangazi yake, polisi waliwakamata watu kadhaa na kuwapeleka kituo cha polisi cha Oysterbay.

Amesema akiwa kituoni hapo, waliulizwa kama wanataka kwenda msalani na wakati anakwenda polisi wawili walimsindikiza na mmoja alimtaka ajiongeze.

Amebainisha kuwa askari mmoja alimsachi mfukoni na kuchukua Sh12,700 huku akimtaka aondoke bila kugeuka nyuma. Amesema alibaki na Sh200 mfukoni na alilazimika

kutembea kwa miguu kutoka kituoni hapo hadi zilipo hosteli za chuo hicho, umbali wa takribani kilomita 10.

Kahumbi amesema walipokuwa katika kituo hicho cha polisi Osterbay askari waliwapiga kwa kutumia mikanda.

Amesema askari mwingine alimpa ngoma mmoja kati ya waliokamatwa na kumtaka apige ngoma, kuwalazimisha waimbe wimbo wenye maneno Dola si lelemama.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika; naibu katibu mkuu-Zanzibar, Salum walimu na Dk Vicent Mashinji.

Wengine ni wabunge Ester Bulaya (Bunda); Halima Mdee (Kawe), Esther Matiko(Tarime Mjini; John Heche (Tarime Vijijini) na Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini).

Mashtaka yao ni kula njama,  kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji jinai kati ya Februari 1 na 16, 2018.

Chanzo: mwananchi.co.tz