Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Akina Mbowe kutetewa na mashahidi 200

80827 Pic+mbowe Akina Mbowe kutetewa na mashahidi 200

Mon, 21 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Viongozi tisa wa Chadema wanaokabiliwa na mashtaka 13, yakiwemo ya uchochezi na kushawishi kutenda jinai, watatumia zaidi ya mashahidi 200 baada ya mahakama kukataa maombi yao na kuamuru waanze kujitetea.

Pia washtakiwa hao wameomba kupatiwa mkanda wa video wa tukio hilo ili wauchunguze kabla ya kuanza utetezi.

Washtakiwa hao, akiwemo mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe wameshtakiwa kwa kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji jinai kati ya Februari mosi na 16, 2018 jijini Dar es Salaam.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya kupitia hoja za upande wa utetezi waliotaka mashahidi ndio waanze kutoa ushahidi kabla ya washtakiwa, ombi ambalo lilipingwa na upande wa mashtaka.

Akitoa uamuzi huo, Hakimu Simba alisema washtakiwa walikutwa na kesi ya kujibu na matakwa ya sheria yanaelekeza mshtakiwa kuanza kujitetea dhidi ya mashtaka yake, ambayo anasomewa upya.

“Ni utaratibu wa kawaida washtakiwa kuanza kujitetea kabla ya mashahidi, hivyo sioni tatizo washtakiwa wakianza kujitetea licha ya upande wa mashtaka kutotoa sababu za kutosha za kwa nini wasianze na mashahidi,’’ alisema.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Baada ya uamuzi huo, wakili wa utetezi, Peter Kibatala alisema wamekubaliana na uamuzi huo na kuomba muda wa kutosha wa kuandaa washtakiwa hao na kuitaka mahakama iwapatie wiki tatu.

Kibatala alisema kuna barua waliandika kwa mfawidhi wa mahakama hiyo wakiomba kupatiwa vielelezo ikiwemo video inayoonyesha tukio la maandamano ili waweze kujiandaa na utetezi hasa katika vipengele vya maneno ambayo washtakiwa wanadaiwa kuyasema.

Alisema pia wanauhitaji mkanda huo wa video waupeleke kwa wataalam kuuchunguza kwa kuwa wana wasiwasi kuwa umehaririwa.

Kibatala alisema wanakusudia kuita mashahidi wasiopungua 200 kwenye kesi hiyo, wakiwa ni watu waliohudhuria mkutano wa Chadema uliosababisha viongozi hao kushtakiwa.

Alisema ili washtakiwa hao waweze kujitetea kikamilifu, lazima wapewe vielelezo hivyo na muda wa kutosha kwa sababu wao ndio wanaodaiwa kusema hayo maneno.

Akijibu hoja hizo, wakili wa Serikali, Faraja Nchimbi alisema mahakama ilitoa uamuzi kuwa washtakiwa wana kesi ya kujibu Septemba 12, takribani mwezi mmoja na siku kadhaa sasa na hivyo walitakiwa kuanza maandalizi ya utetezi.

Kuhusu vielelezo, Nchimbi alisema bahati mbaya suala hilo linashughulikiwa na upande wa utetezi na mahakama na kwamba upande wa mashtaka hawakupatiwa nakala, hivyo aliomba wapewe nakala ili wajue ni kitu gani kinaendelea, hasa ukizingatia wingi wa mashahidi wao.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 21, atakapotoa uamuzi kuhusu muda ulioombwa na upande wa utetezi.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya Kibatala kueleza kuwa katika kesi yao hiyo wataita mashahidi wengi.

Washtakiwa hao wanaanza kutoa utetezi wao baada ya mashahidi wanane wa upande wa mashtaka kutoa ushahidi wao na mahakama kuwaona wana kesi ya kujibu.

Washitakiwa katika kesi hiyo, mbali na Mbowe ni Salum Mwalimu, ambaye ni naibu katibu mkuu Zanzibar, John Mnyika (naibu katibu mkuu Bara), John Heche (mbunge wa Tarime Vijijini), Halima Mdee (mbunge Kawe), na Ester Bulaya (mbunge wa Bunda).

Wengine ni Mchungaji Peter Msigwa, ambaye ni mbunge wa Iringa Mjini, Esther Matiko (mbunge wa Tarime Mjini), na katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji.

Washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji jinai kati ya Februari 1 na 16, 2018, Dar es Salaam.

Katika kipindi hicho, Chadema ilikuwa ikishiriki uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kinondoni ikiwakilishwa na Mwalimu na mashtaka hayo yalitokana na tukio lililotokea eneo la Kinondoni Mkwajuni ambako risasi ilifyatuliwa na kumpiga kichwani mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini na kusababisha kifo chake.

Chanzo: mwananchi.co.tz