Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ahukumiwa kifungo kwa kumuibia marehemu mumewe

Jelaa2.png Ahukumiwa kifungo kwa kumuibia marehemu mumewe

Fri, 30 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu, Ofisa Utamaduni Manispaa ya Lindi, Makalaghe Shekhalaghe Mkindi (50) kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela au kulipa faini Sh7 milioni baada kupatikana na hatia ya wizi wa Sh198 milioni za marehemu mumewe aitwaye Suleiman Mohamed.

Mshtakiwa anadaiwa kuchukua fedha hizo kwa nyaraka tofauti kupitia ATM, baada ya mume wake kufariki dunia.

Pia Mahakama hiyo imeamuru kuchukuliwa nyumba ya Mkinda iliyopo Msavu mkoani Morogoro na kuingizwa katika Mirathi namba 23 ya mwaka 2022, iliyofunguliwa Mahakama ya Mwanzo Sinza.

Hukumu hiyo imetolewa leo jioni, Juni 30, 2023 na Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutolewa hukumu.

Hakimu Kabate amesema ameridhishwa na ushahidi wa mashahidi, wanne wa upande wa mashtaka waliotoa dhidi ya mshtakiwa huyo, hivyo amemtia hatiani kama alivyoshtakiwa.

Akipitia ushahidi, Hakimu Kabate amesema kukiri kwa mshtakiwa katika utetezi wake na ushahidi wa taarifa za kibenki uliowasilishwa mahakamani hapo, unaifanya mahakama isiwe na maswali ya ziada ya kujiuliza juu ya ukweli kuwa mtuhumiwa aliiba kiasi hicho cha fedha.

"Ushahidi uliotewa na wa mashahidi wanne wa upande wa mashitaka umeeleza jinsi ambavyo fedha ilikuwa ikitolewa benki na mshitakiwa baada ya kifo cha mume wake bila kufungua shauri la Mirathi," amesema Hakimu Kabate na kuongeza;

"Mshitakiwa mwenyewe alikiri kutoa na kutumia fedha kwa matumizi binafsi na kutoa sadaka katika Masjid Huddah mkoani Lindi, sasa sijui alikuwa anajua kama ni kosa kutoa fedha za marehemu wakati hajafungua mirathi au alikuwa anafanya makusudi."

Kutokana na hali hiyo, mahakama imeegemea katika kifungu cha 258 na 265 vya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Alisema vifungu hivyo vinaeleza wazi wizi ni nini na mazingira gani ambayo yanatafsiriwa kama wizi.

Amesema kutokana na utetezi wa mshitakiwa alioutoa kabla ya hukumu kuwa sehemu ya fedha alizoiba alizitoa kama sadaka katika msikiti na shahidi wake alieleza jinsi ambavyo walinufaika na msaada huo mahakama imeona impunguzie adhabu.

"Mahakama imeshawishika na hoja za wakili wa utetezi alizozita kupitia kifungu cha 27(2) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo 2022, kuwa mshtakiwa ni mkosefu kwa mara ya kwanza na anaomba apewe adhabu ndogo ambayo ni kulipa faini na sio kifungo, hivyo nina wiwa kumpa adhabu ya kulipa faini," anasema Hakimu Kabate.

Akiendelea kutoa hukumu, Hakimu Kabate amesema, amezingatia mshtakiwa hana kumbukumbu za makosa ya nyuma pia mshitakiwa ana familia inayomtegemea ikiwemo watoto yatima na anamhudumia baba yake mzazi ambaye ni mgonjwa wa muda mrefu.

"Hivyo Mahakama hii inahukumu kifungo cha mwaka mmoja jela au kulipa faini ya Sh7 milioni na kukabidhi nyumba yako iliyopo Msavu mkoani Morogoro yenye thamani ya Sh70 milioni ili iingie katika mirathi," amesem Hakimu Kabate na kuongeza;

"Na ikigundulika ni uongo huna nyumba Msavu, utaletwa hapa mahakamani utashtakiwa kwa kutoa taarifa za uongo na kughushi, hivyo mahakama inakutaka utoe ushirikiano katika nyumba yako iliyopo huko Morogoro ili ijumuishwe katika mirathi namba 53/2021 iliyofunguliwa katika Mahakama ya Mwanzo Sinza," amesema Hakimu Kabate.

Awali, upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili Agness Mtunguja akisaidiana na Eva Kassa, uliomba mahakama itoe adhabu kali ili iwe somo na fundisho kwa mshitakiwa na jamii inayomzunguka.

Katika utetezi wake mshtakiwa aliomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa amejutia kosa lake.

Katika kesi msingi, Shekalaghe alikuwa anakabiliwa na kesi ya jinai namba 122/2021.

Anadaiwa kati ya Januari, 2020 na Juni 2020, katika maeneo tofauti katika Mkoa wa Dar es Salaam, mshtakiwa kwa makusudi aliiba Sh198, 750, 000 kutoka katika akaunti ya NMB iliyokuwa ikimilikiwa na marehemu mume wake aliitwaye, Suleiman Mohamed.

Anadaiwa kuiba fedha hizo kwa nyakati tofauti kupitia ATM, wakati alijua mumewa ameshafariki dunia na kwamba anatakiwa kufungua mirathi.

Inadaiwa kuwa Mkinda alikuwa mke mdogo ambapo mume wake alikuwa ameoa wake watatu na kila mke alikuwa amemjengea nyumba moja.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live