Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Afungwa miaka mitatu kwa kuomba laki mbili kwa mgonjwa

1944 Jail 660x400 Miaka mitatu jela kwa kuomba laki mbili kwa mgonjwa

Mon, 23 Aug 2021 Chanzo: Nipashe

MAHAKAMA ya Hakimu Mfawidhi Wilaya ya Igunga, mkoani Tabora imemhukumu muuguzi wa hospitali ya wilaya hiyo, Wallace Kaziri (53), kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya Sh. 500,000 baada ya kumtia hatiani kwa makosa ya kuomba na kupokea rushwa ya Sh. 200,000 kwa mgonjwa.

Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Wilaya ya Igunga, Mazengo Joseph, alidai kuwa mshtakiwa huyo alikuwa akikabiliwa na mashtaka matatu ya rushwa.

Mbele ya Hakimu wa Wilaya, Godfrey Rwekit, mwendesha mashtaka alidai shtaka la kwanza la kuomba rushwa, Oktoba 30, mwaka 2019, mshtakiwa akiwa muuguzi wa zamu katika hospitali ya wilaya hiyo, aliomba rushwa ya Sh. 200,000 kutoka kwa Kasemba Bundala, ili aweze kumpatia dawa ya ugonjwa wa kifua kikuu aliyekuwa amelazwa katika hospitali hiyo, Bugumba Luhende, ambaye ni mama wa Bundala.

Pia katika shtaka la pili la kupokea rushwa ya Sh. 50,000, Oktoba 30, 2019, mshtakiwa huyo alipokea kwa njia ya simu ya mkononi Sh. 50,000 kama malipo ya awali ya Sh. 200,000 alizoomba.

Mwendesha mashtaka huyo alidai kwamba katika shtaka la tatu la kupokea rushwa ya Sh. 50,000, Novemba 1, 2019, mshtakiwa alipokea kiasi hicho kama malipo mengine ya awali ya Sh. 200,000 na kufanya jumla ya fedha alizopokea kuwa Sh. 100,000.

Kwa mujibu wa Mazengo mshtakiwa huyo alitenda makosa hayo kinyume na kifungu cha 15 (a) na (2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11/2007.

Hata hivyo, baada ya kusomewa mashtaka yote, mshtakiwa alikana na upande wa jamhuri ulipopeleka mahakamani jumla ya mashahidi tisa pamoja na vielelezo 12, ushahidi ulimtambua mshtakiwa huyo.

Mwendesha mashtaka huyo alidai kuwa baada ya mahakama kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, Hakimu Rwekiti alisema ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri umethibitisha bila kuacha shaka yoyote kwamba mshtakiwa ametenda makosa hayo.

Mazengo alisema kwamba kutokana na ushahidi huo mahakama hiyo ilimwona mshtakiwa, Wallace Kaziri, ana hatia na kumhukumu adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya Sh. 500,000. Mshtakiwa alifanikiwa kulipa faini hiyo na kuachiwa huru.

Chanzo: Nipashe