Mahakama ya Wilaya Nkasi mkoani Rukwa imemhukumu kifungo cha maisha jela, Peter Malema (21) baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka minne.
Kijana huyo ni Mkazi wa Kijiji cha Nkundi kilichopo katika Kata ya Kipande wilayani Nkasi.
Kumbukumbu zilizopo mahakamani hapo zinaonesha kuwa mshatakiwa huyo aliwahi kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela lakini alikata na kushinda rufaa na kuachiwa huru.
Akitoa hukumu jana, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya, Benedict Nkomola alisema mahakama hiyo imefikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha na ushahidi uliotolewa kuwa mshtakiwa alitenda uhalifu huo.
Akifafanua alisema kuwa mshtakiwa alitiwa hatiani kwa kutenda kosa hilo chini ya kifungu cha sheria cha 130 (1) na (2)(e) na kifungu cha 131 (3) sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.
Upande wa mashitaka ukiongozwa na Mwendesha Mashtaka, Denis Chagike akisaidiwa na Sedrick Mashauri, alidai mahakamani hapo kuwa mshitakiwa alitenda kosa Machi 23, 2021 katika Kijiji cha Nkundi ambapo alimbaka mtoto huyo wa miaka minne na kumsababishia maumivu.
Sambamba na hilo, waendesha mashitaka hao waliiambia mahakama hiyo kuwa ni kosa lake la pili la ubakaji ambapo katika kosa la kwanza aliwahi kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na aliachiwa huru baada ya kushinda rufaa.
Hivyo waliiomba mahakama itoe adhabu kali iwe ni fundisho kwa watu wengine wenye nia ya kutaka kufanya vitendo kama hivyo. Upande huo wa mashitaka uliita mashahidi nane.