Dar es es Salaam. Mkazi wa Upanga jijini Dar es Salaam, Joash Nyamasangara amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka manne likiwemo la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kiasi cha Sh50 milioni.
Akisoma hati ya mashtaka leo Jumanne Oktoba 15, 2019 wakili wa Serikali, Candid Nasua amedai mshtakiwa huyo anakabiliwa na shtaka la uhujumu uchumi kesi Namba 111/2019.
Nasua amedai tarehe zisizofahamika mwaka 2018 maeneo ya Jiji la Dar es Salaam alighushi nyaraka za kutolea mizigo bandarini namba B/L Eukoxit 1524084 ya Machi17, 2018 ya kampuni ya Delta Earth Moning Unganda akijua siyo kweli.
Katika shtaka la pili Agosti 13, 2018 eneo la Samora jijini Dar es Salaam alighushi nyaraka za mizigo bandarini B/L Eukoxit 1524084 ya Machi17, 2018 ya kampuni ya Delta Earth Moning Unganda huku akijua nyaraka za uongo.
Shtaka la tatu, tarehe hiyo hiyo na maeneo hayo alijiingizia kiasi cha Sh50 milioni mali ya Ersal Yazici kwa kudanganya kuwa anamuuzia gari la kubebea winchi (truck Crane) huku akijua siyo kweli.
Shtaka la mwisho tarehe hiyo hiyo na maeneo hayo alitakatisha Sh50 milioni kutoka kwa Ersal Yazici ikiwa ni zao la makosa tangulizi ya kujipatia fedha kwa ajili ya udanganyifu
Pia Soma
- Rais Zuma kukata rufaa dhidi ya kesi yake ya ufisadi
- Profesa Ndalichato atoa maagizo kwa katibu mkuu wizara ya elimu
- Upepo wajeruhi wawili, nyumba 49 na makanisa yaezuliwa Butiama
- Tasupa watoa masharti ununuzi wa alizeti Tanzania
Hakimu Mkazi, Vick Mwaikambo amesema kwa kuwa shtaka hilo la uhujumu uchumi hivyo mshtakiwa haruhusiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hii haina mamlaka .
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 28, 2019.