Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Afariki dunia akikimbizwa na polisi akisafirisha mirungi

Vijiji Vitatu Vyaacha Kulima Mirungi Same.png Afariki dunia akikimbizwa na polisi akisafirisha mirungi

Sun, 17 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la Mkacha Mohamed (35), mkazi wa Soya wilaya ya Chemba Mkoani Dodoma, amefariki dunia baada ya kuanguka na pikipiki akiwa na mwenzake wakiwakimbia Polisi wa Kibaya waliokuwa kwenye doria kijiji cha Namelock.

Vijana hao walikuwa wanasafirisha shehena ya madawa ya kulevya aina ya mirungi bunda 250 sawa na kilo 119.

Tukio hilo limetokea leo Jumapili Septemba 17, 2023 katika kijiji cha Namelock Kata ya Namelock Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Manyara, ACP George Katabazi amethibitisha kutokea tukio hilo na kumtaja marehemu huyo kuwa ni Mkacha Mohamed, aliyekuwa amepakia mwenzake aliyejulikana kwa jina la Nasibu Yahaya (23) ambaye yeye amenusurika kifo.

"Marehemu Mkacha Mohamed Mkacha (35) ndiye aliyekuwa dereva wa pikipiki iliyopata ajali hiyo ambayo pia alibeba abiria huyo na shehena ya madawa ya kulevya aina ya mirungi.

Pikipiki hiyo ilipasua tairi ya mbele wakati wakifukuzana na askari Polisi wa Kibaya ambao waliokuwa kwenye doria baada ya kuhisi kuwa watu hao walikuwa wamebeba magendo na waliposimamishwa na Askari hao hawakusimama ndipo wakaanza kufukuzana kisha pikipiki yao kupasua tairi na kuanguka na kusababisha kifo hicho," amesema ACP Katabazi.

Amesema mwenzake aliyekuwa amepakiwa nyuma, hakuumia na hana hata mchubuko lakini dereva alipoteza maisha hapo hapo na mwili wake umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Wilaya ya Kiteto.

"Mwili wa marehemu amehifadhiwa chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Wilaya ya Kiteto na Nasibu Yahaya Bakari (23) aliyekuwa amebebwa kwenye pikipiki hiyo hakuumia na anaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi Kiteto kwa upelelezi zaidi," amesema.

Aidha Kamanda Katabazi amesema madawa hayo ya kulevya yalikuwa yanasafirishwa kwenda Wilaya ya Chemba Mkoa wa Dodoma kwa usafiri wa pikipiki aina Sinoray ambayo haikuwa na namba za za usajili.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live