Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aeleza mshitakiwa alivyosalimisha fedha ‘alizokwapua’ Benki ya NBC

Hukumu Pc Data Aeleza mshitakiwa alivyosalimisha fedha ‘alizokwapua’ Benki ya NBC

Fri, 5 May 2023 Chanzo: Habarileo

Ofisi wa Polisi kutoka Kituo cha Oysterbay, Inspekta Democracy Nivaco ameieleza mahakama namna mshitakiwa Charles Matanya alivyosalimisha kiasi cha Sh milioni 10 kati ya milioni 61 alizoziiba kutoka Benki ya NBC, tawi la Samora jijini Dar es Salaam.

Ofisa huyo pia alieleza namna walivyokamata gari aina ya Toyota Premio lenye namba T 360 BNA ambalo mshitakiwa alikuwa amelinunua kutokana na fedha hizo.

Hayo yalijiri jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate wakati Inspekta Democracy alipokuwa akitoa ushahidi.

Democracy ambaye ni shahidi wa sita katika kesi hiyo alieleza kuwa Juni 21, 2018 alipokea jalada la kesi ya wizi kutoka kwa mkuu wake wa kazi lenye jina la mshitakiwa Charles Matanya ili afanye uchunguzi.

Alidai alianza uchunguzi kwa kumhoji mshitakiwa ambaye alikiri kuiba fedha hizo, alidai baada ya kukiri mshtakiwa aliomba afanye mawasiliano na ndugu zake na alimruhusu.

“Alifanya mawasiliano na kaka yake aliyemtambulisha kwa jina la Zakaria Matanya ambaye alikuja baada ya muda mfupi akiwa na Sh milioni kumi, alitueleza kuwa Charles alimwagiza azilete,” alisema.

Aliendelea kudai kuwa mshitakiwa alikiri kumwagiza kaka yake azipeleke fedha hizo na yeye alizikamata na kuandaa hati ya ukamataji ambayo ilisainiwa na mshitakiwa pamoja na mashahidi ambao ni maofisa wa polisi aliokuwa nao wakati wa kumhoji.

Alidai baada ya mahojiano alipata taarifa kuwa mshitakiwa alinunua gari katika yadi ya kuuza magari aliyoitaja kwa jina la World iliyoko maeneo ya Kinondoni Morocco.

Alidai alikwenda katika yadi hiyo na kukutana na Mkurugenzi wake aliyemtaja kwa jina moja la Othman ambaye alikiri kupokea Sh milioni 14 kutoka kwa Matanya ili amuuzie gari hiyo.

Inspekta Democracy aliendelea kudai kuwa baada ya kuthibitishiwa hilo alilikamata gari hilo na kuandaa hati ya ukamataji ambayo alijaza nyaraka zote muhimu ikiwemo kadi ya gari na risiti ya mauzo.

Katika kesi hiyo, Matanya anashtakiwa akidaiwa kuiba fedha Juni, 2018 kwa alipoingiziwa kimakosa Sh milioni 360 kwenye akaunti yake iliyoko katika benki ya NBC tawi la Samora, Dar es Salaam.

Iliendelea kudaiwa kuwa baada ya kuingiziwa fedha hizo kimakosa, Matanya hakutoa taarifa kwa benki na badala yake alianza kuzitoa na kuzitumia hadi alipokamatwa akitaka kutoa Sh milioni 20 katika tawi la Kinondoni. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Mei 26, 2023.

Chanzo: Habarileo