Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Adhabu ya familia ‘yasababisha’ kifo

Hukumu Pc Data Adhabu ya familia ‘yasababisha’ kifo

Fri, 28 Oct 2022 Chanzo: mwanachidigital

Mzee mwenye umri wa miaka 90 na wanawe watatu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za mauaji ya ndugu yao wakimtuhumu kushiriki kikao cha usuluhishi akiwa amelewa.

Taarifa kutoka eneo la tukio zinaeleza watuhumiwa hao wanadaiwa kumwadhibu ndugu yao kwa kumchapa kwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili, wakimtuhumu kuwaaibisha kwa kushiriki kikao cha usuluhishi akiwa amelewa.

Ndugu hao wanaoshikiliwa na polisi wakituhumiwa kumuua ndugu yao, Simon Leshoo (35) ni Leshoo Kisoki Mollel (90) ambaye ni baba mzazi na wanawe, Simon Leshoo (30), Baraka Leshoo (38) na Abedi Leshoo (15), wote wakiwa ni wakazi wa kijiji cha Munge wilayani Siha, mkoani Kilimanjaro.

“Jamaa ni mpiga maji sana, sasa tunavyosikia kulikuwa na kikao cha usuluhishi, sijajua ni cha ndugu au kilihusisha pia na watu wengine nje ya familia. Hiyo siku jamaa alikuja yuko tungi (amekunywa) na iliwaudhi ndugu,” chanzo kilichokataa jina lake kuandikwa gazetini kilidai.

Chanzo hicho kimedai kuwa kitendo hicho kilimkera baba yake pamoja na ndugu wengine na ndipo walipokubaliana kumwadhibu kama njia ya kumuonya asirudie kufanya kitendo cha aina hiyo.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Munge, Isack Kalanga Mollel alisema siku ya tukio saa 2:47 asubuhi, alipata taarifa kutoka kwa balozi wa eneo hilo, kuwa kijana huyo amefariki baada ya kuchapwa fimbo sehemu mbalimbali.

“Tukio hili limetokana na masuala ya kifamilia. Familia ilimchapa fimbo hadi kufariki, walikuwa wakimuadhibu kutokana na tatizo la ulevi. Walimfunga kamba wakamchapa fimbo akafariki dunia,” alidai mwenyekiti huyo.

Alisema marehemu ameacha wake wawili na watoto na wanalilaani tukio hilo kwa sababu ni la kikatili.

RPC aeleza tukio lilivyokuwa

Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Simon Maigwa alisema kuwa tukio hilo lilitokea Oktoba 24, 2022 saa 2:47 asubuhi ambapo baba mzazi na wanawe watatu, waliamua kujichukulia sheria mkononi kumwadhibu ndugu yao.

Alisema siku ya tukio, mwili wa marehemu ulikutwa katika nyumba ambayo ujenzi wake haujakamilika (pagale) ukiwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili baada ya kudaiwa kuchapwa fimbo na watuhumiwa.

Alifafanua kuwa upelelezi wa awali umebaini siku hiyo saa 12:00 asubuhi, watuhumiwa wakiongozwa na Leshoo Kisoki Mollel walifika nyumbani kwa marehemu na kumuita kwa ukali na kumtaka atoke nje.

“Walikuwa wakimwambia kuwa amewaaibisha kwenye kikao walichofanya cha usuluhishi kwamba alikuwa amelewa pombe na hivyo anastahili adhabu. Walimchukua na kuondoka naye,” alisema kamanda Maigwa na kuongeza:

“Kisha walimchapa kwa kutumia fimbo sehemu mbalimbali za mwili na ndipo umauti ulimkuta. Mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi na daktari na kubaini chanzo cha kifo ni kupasuka bandama na pingili za mgongo vilivyosababishwa na kupigwa na kitu butu”.

Alisema upelelezi zaidi kuhusiana na tukio hilo unaendelea, ikiwa ni pamoja na kuwatafuta na kuwakamata wote waliohusika kwenye tukio hilo, pasipo kufafanua kama kuna ndugu au watu baki walioshiriki tukio hilo.

Kamanda alitoa wito kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na kuitaka jamii kuwatumia viongozi wa dini, Serikali na polisi kushughulikia masuala ya kimaadili katika jamii kuliko kujichukulia sheria mkononi.

Chanzo: mwanachidigital