Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Adakwa na vipande 18 vya meno ya tembo

0135646c1334e7e27967ee13f592ad12 Adakwa na vipande 18 vya meno ya tembo

Fri, 15 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Polisi mkoani Morogoro kwa kushirikiana na Jeshi la Uhifadhi Hifadhi ya Taifa ya Nyerere linamshikilia mkulima na mkazi wa Duthumi Wilaya ya Morogoro, Semeni Issa (49), kwa tuhuma za kupatikana na vipande 18 vya meno ya tembo akiwa ameyahifadhi ndani ya kiroba.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Fortunatus Musilimu alisema jana kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa Aprili 8, mwaka huu saa 10 jioni Mgeta Wilaya ya Mvomero.

Kamanda Musilimu alisema Issa alikamatwa kutokana na kupata taarifa za msiri wao na hivyo kumkamata ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Nyerere akiwa na meno ya tembo vipande 18 vikiwa ndani ya kiroba, kikiwa na uzito wa kilo 61 na thamani yake haijafahamika mara moja.

Alisema mtuhumiwa alipohojiwa mbele ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyandira kinachopakana na Hifadhi ya Taifa ya Nyerere alikiri kupatikana na meno hayo, na kwa siku tofauti aliingia hifadhini kuua tembo na kuchukua meno hayo na kuyahifadhi.

Alisema mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa na baada ya mahojiano kukamilika atafikishwa mahakamani.

Alitoa mwito kwa wananchi kuacha kuvamia hifadhi na kuua wanyama na kwenda kufanya biashara haramu, badala yake wafanye kazi na biashara zitakazowapatia kipato halali.

Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, Halid Mngofi alisema Jeshi la Uhifadhi la Tanapa katika hifadhi hiyo kwa kushirikiana na Polisi wameanza kufanya doria ya pamoja ili kukabiliana na viashiria vya uhalifu wa ujangili wa wanyamapori.

Alisema vipande vya meno ya tembo vilivyokamatwa ni sawa na tembo watano wameuawa, na inaonesha yalihifadhiwa miaka mitatu nyuma na mtuhumiwa alikuwa akitafuta soko.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live