Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Adakwa JNIA na kilo 17 za heroin

5d96936f90f9f33007167a0894247456.jpeg Baadhi ya mizigo na vifurushi alivyokutwa navyo mtuhumiwa

Tue, 3 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Raia wa India, Paokholen Lhungdim (23) amekamatwa na Jeshi la Polisi la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam akiwa na kilogramu 17.40 za dawa za kulevya aina ya heroin. Dawa hizo zilikuwa zikisafirishwa kutoka Harare nchini Zimbabwe kupelekwa Mumbai nchini India.

Kamanda wa Polisi Viwanja vya Ndege Tanzania, Jeremia Shila alisema jana kuwa kijana huyo alikamatwa Aprili 29 mwaka huu saa 2 usiku katika jengo la tatu la abiria kwenye eneo la ukaguzi wa mizigo ya abiria wanaosafiri kwenda nje ya nchi. Kamanda Shila alisema mtuhumiwa aliwasili nchini kwa Ndege ya Air Tanzania (ATCL) saa 2 usiku ikitoka Harare Zimbabwe na alikuwa anatarajia kuunganisha safari yake kwenda Mumbai India kwa ndege nyingine ya ATCL.

Alisema mizigo ya kijana huyo ilishushwa na kukaguliwa upya kwa ajili ya kuendelea na safari ndipo aligundulika alibeba dawa za kulevya aina ya heroin.

“Ukamataji huu ni mkubwa mara ya mwisho tulikamata kilogramu 13 katika uwanja wa JNIA na kama dawa hizo zingefanikiwa kusafirishwa kuelekea Mumbai wangeharibu nguvu kazi ya India, yangesababisha athari kubwa,” alisema Kamanda Shila na akaongeza: “Mtuhumiwa alikuwa amejipanga, kama hauna uwezo wa kufuatilia huwezi ukagundua jinsi alivyoshonea dawa za kulevya kwenye mabegi yote mawili.”

Alisema mtuhumiwa alikuwa na mabegi yanayofanana na kila begi aliweka bahasha mbili ambazo alikuwa amezifunga kwa ustadi ndiyo maana alikotoka alipita bila kubainika. Kamanda Shila alisema wanaosafirisha dawa za kulevya wamekuwa wakibuni mbinu kufanikisha malengo yao lakini polisi JNIA walimbaini mtuhumiwa huyo kwa kuwa walipata mafunzo.

Katika hatua nyingine Jeshi la Polisi JNIA walimkamata raia wa China, Dong Weijun (44) akiwa na vidani 10 na bangili moja vilivyotengenezwa kwa meno ya tembo vyenye uzito wa gramu 110. Kamanda Shila alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa saa 4 asubuhi katika eneo la kuondokea abiria sehemu ya ukaguzi wa mizigo.

Alisema kijana huyo alikuwa akisafiri kwa ndege ya Shirika la Qatar kwenda Bangkok nchini Thailand. Alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa na bangili nyingine moja iliyotengenezwa na manyoya ya mkia wa tembo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live