Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Adaiwa kujiua kwa kunywa sumu ya kupulizia mikorosho

Poisons And Solvents.jpeg Adaiwa kujiua kwa kunywa sumu ya kupulizia mikorosho

Wed, 27 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Aden Bakari (59) mkazi wa Kijiji cha Nambeleketela, mkoani Mtwara amefariki dunia wakati akiwahishwa hospitalini Desemba 24, 2023 baada ya kunywa sumu ya kupulizia mikorosho.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, ACP Nicodemus Katembo amethibitisha kifo hicho, akiitaja dawa hiyo kwa jina la Macrom, akisema ndani yake ina viambata vya sumu.

“Kifo hicho kimetokea baada ya marehemu kunywa sumu ya kupulizia mikorosho aina ya Macrom inayodaiwa kuwa na viambata vyenye sumu, Jeshi la Polisi bado lipo katika uchunguzi kujua sababu zaidi za kifo hicho," amesema Katembo.

Akizungumza leo Desemba 27, 2023 kijijini hapo, mke wa marehemu, Somoe Nalumanga amesema kuwa alipotoka shambani alifika nyumbani na kumkuta mume wake akiwa amelala kitandani, huku kukiwa na harufu ya dawa ya kupuliza mikorosho.

“Niliporejea nyumbani nilikuta mlango umefungwa kwa ndani, nikachukua mwiko nikafungua na nilipoingia chumbani nilishangaa kuona kopo chini ya kitanda, huku mume wangu amelala kitandani na pembeni ya kopo naona maji maji na harufu ya dawa ya mikorosho.

"Nilijaribu kumuita lakini akawa anaitika kwa sauti ya chini tofauti na nilivyomzoea huku akionekana hana nguvu, niliogopa nikaamua kuomba msaada kwa majirani kwa kuwa nilihisi amekunywa ile dawa ya mikorosho kutokana na mazingira nilivyoyaona,” amesema Nalumanga

Naye mpwa wa marehemu, Usu Saidi Mchuuzi amesema kuwa alipata taarifa baada ya kupigiwa simu, ambapo aliwahi eneo la tukio na kumkuta marehemu akiwa anatokwa na povu mdomoni huku akiwa hawezi kuongea.

“Nilipigiwa simu ili kutoa msaada nilipofika nilimkuta marehemu akitoa povu mdomoni na alikuwa hawezi tena kuongea na ndipo tulimuwahisha Hospitali ya Ligula na baadaye tulipokea taarifa kuwa amefariki dunia,” amesema Mchuuzi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live