Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Adaiwa kujinyonga, kisa wazazi kumchukua mpenzi wake

Kifo Kifo Mauiaji.png Adaiwa kujinyonga, kisa wazazi kumchukua mpenzi wake

Thu, 18 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkazi wa Mtaa wa Idundilanga, wilayani Njombe, Venance Haule (24) anadaiwa kujinyonga kwa kile kinachoelezwa mwanamke aliyekuwa akiishi naye kuchukuliwa na wazazi wake wakati bado anampenda.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga, ameeleza hayo leo Januari 18, 2024 alipozungumza na waandishi wa habari na kusema Haule amejinyonga kwa kutumia pazia chumbani kwake.

Amesema tukio hilo limetokea jana, Januari 17, 2024 asubuhi na inadaiwa marehemu alikuwa akisumbuliwa na ndugu wa mwanamke huyo wakishinikiza amlipie mahali kwa vitisho kuwa ni mwanafunzi.

Kamanda Banga amesema mwanamke aliyekuwa akiishi na marehemu huyo alikuwa mwanafunzi, aliacha shule mwaka 2023 akiwa kidato cha tatu.

“Mwaka 2024 alitakiwa kuwa kidato cha nne, lakini kwa kutokuwepo shuleni kwa muda mrefu walimfukuza, kwa hiyo si mwanafunzi tena,” amesema Banga.

Amesema kulingana na maelezo ya mwanamke aliyekuwa akiishi na marehemu ni kuwa ndugu zake walikuwa wanakwenda kwa mwanamume huyo kujitambulisha kuwa wao ni askari na wamefungua kesi kwamba anaishi na mwanafunzi.

Kamanda huyo amesema lengo lao ilikuwa Haule atoe fedha za hongo au kutoa mahali ambapo inadaiwa hivi karibuni ndugu hao wa mwanamke walikwenda kumchukua ndugu yao na kumrudisha nyumbani.

“Kimsingi yalikuwa mashinikizo kwamba kijana yule aende akatoe mahali, lakini huyu kijana shughuli yake kubwa ilikuwa fundi ujenzi, kwa hiyo uwezo wake ulikuwa si mkubwa kifedha, kwa hiyo katika hali kama hiyo alikuwa anampenda huyo mwanamke,” amesema Kamanda Banga.

Amesema kwa maelezo aliyoyaacha marehemu kupitia ujumbe wa barua aliyoiandika ni kuwa mwanamke huyo ni mjamzito na mtoto atakayezaliwa amtunze.

Mmiliki wa nyumba aliyopanga marehemu enzi za uhai wake, Sarah Magehema amesema Haule ameishi hapo kwa muda wa miezi sita na alikuwa anaona anaishi na mwanamke huyo kwa kujifungia ndani muda mwingi.

“Kwa kweli tukio hilo siwezi kujua kwa undani zaidi kwa sababu mkewe alikuwa ameondoka Jumamosi, hakuniaga anakwenda wapi, ila Jumatatu mumewe aliniambia jioni kwamba ‘mwenzangu ameondoka hapa bila ya kuniaga’,” amesema Magehema.

Amesema kwa kipindi chote hicho hakujua kuwa marehemu alikuwa anaishi na mwanafunzi, lakini baada ya kutokea tukio hilo ndiyo akasikia taarifa hiyo.

Kwa upande wake, kaka wa marehemu, Wilson Haule amesema hayupo tayari kuzungumzia chochote kuhusu tukio hilo.

“Siwezi kuzungumzia chochote kwa sababu mimi mwenyewe nimesikia taarifa asubuhi hii, kwa hiyo sifahamu chanzo,” amesema Haule.

Mwanasheria kutoka kituo cha msaada wa kisheria, Njopace Eddy Kibona amesema wananchi wanapaswa kujua suala la kujinyonga ni kosa kisheria hata kama umekumbana na tatizo kubwa kiasi gani.

“Hautakiwi kufanya tukio kubwa kama hilo kwa sababu ni kinyume cha sheria za nchi lakini pia ni kinyume na maadili ya kidini ambayo mtu amekulia,” amesema Kibona.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live