Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Adaiwa kuiba mtoto, achoma godoro ionekane kateketea

48516 Pic+jela Adaiwa kuiba mtoto, achoma godoro ionekane kateketea

Wed, 24 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

JESHI la Polisi mkoani Rukwa linamshikilia mwanamke mmoja (jina limehifadhiwa), mkazi wa kijiji cha Msata mkoani Pwani, kwa tuhuma za kumuiba mtoto mwenye umri wa wiki moja na kisha kuchoma godoro alilokuwa amelalia mtoto huyo ili ijulikane ameteketea kwa moto.

Tukio hilo lilitokea Juni 11, majira ya saa 2:30 usiku katika eneo la Namanyere, wilayani Nkasi baada ya mtuhumiwa huyo kumuiba mtoto huyo kwa ndugu yake Samia Ruhusa (35), mkazi wa Namanyere wilayani humo.

Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa, Justine Masejo, alisema siku ya tukio mtuhumiwa alimpigia simu mama wa mtoto huyo na kumwambia kuwa yupo jijini Dar es Salaam, amemtumia fedha za matumizi kupitia mtandao wa simu, aende akazitoe usiku huo ili zimsaidie katika kipindi ambacho amejifungua.

Baada ya mama wa mtoto kuambiwa hivyo aliondoka nyumbani kwake na kumuacha mtoto amemlaza kwenye godoro, ndipo mtuhumiwa anayedaiwa kuwa alikuwa karibu na nyumba hiyo amejificha, aliingia ndani na kuchoma moto godoro alilokuwa amelalia mtoto huyo kwa lengo la kupoteza ushahidi ili idhaniwe kuwa mtoto huyo ameteketea kwa moto na kisha kumchukua na kutokomea naye.

Mama mwenye mtoto aliporudi nyumbani alikuta moto unawake ndani na kuanza kupiga kelele za kuomba msaada, majirani walifanikiwa kuingia ndani na kuuzima moto huo, lakini hawakukuta mwili wa mtoto huyo zaidi ya kukuta kipande cha godoro kikiwa kimeungua.

Kamanda Masejo alisema, mama huyo pamoja na majirani waliamua kwenda polisi kutoa taarifa ya tukio hilo na polisi walianza uchunguzi kwa kuwakamata watu mbalimbali wanaodhaniwa kuhusika katika tukio hilo.

Alisema polisi kwa kushirikiana na wananchi walifanikiwa kumkamata mama huyo akiwa mkoani Pwani, Kijiji cha Msata na alipohojiwa alikiri kufanya tukio hilo la kumuiba mtoto na kutoroka naye, kwa kuwa ametafuta mtoto kwa muda mrefu bila mafanikio ndiyo maana aliamua kwenda kumuiba mtoto huyo wa ndugu yake baada ya kupata taarifa kuwa amejifungua.

Kamanda alisema mtuhumiwa anashikiliwa na polisi na taratibu za kisheria zinafanyika ili afikishwe mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live