Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aburutwa kortini akidaiwa kujifanya Waziri wa Ardhi

Hukumu Pc Data Aburutwa kortini akidaiwa kujifanya Waziri wa Ardhi

Thu, 5 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mshtakiwa Frank Rugeimkamu amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa mashtaka saba, ikiwamo kujifanya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi (wakati huo Angeline Mabula), akilenga kujipatia Sh5.4 milioni kwa njia ya udanganyifu.

Akisoma mashtaka hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swalo, Wakili wa Serikali, Asiath Mzamiru alidai kuwa mshtakiwa huyo anakabiliwa na kosa hilo la udanganyifu ili ajipatie fedha kwa kutumia laini ya simu ya mtu mwingine.

Mzamiru alidai Septemba 2021 mshtakiwa alijifanya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angeline Mabula kwa Furaha Dominick, huku akijua kuwa si kweli.

Katika shtaka la pili inadaiwa kuwa Mei 22, 2022 eneo la Buswelu Wilaya ya Ilemela Mwanza, mshtakiwa alijifanya waziri kwa kutumia ujumbe mfupi kupitia mtandao wa kijamii wa WhatsApp kwa Tabia Mwita huku akijua si kweli.

Pia, inadaiwa katika tarehe isiyojulikana Mei, 2022 eneo la Buswelu Mwanza, mshtakiwa alijifanya Waziri Angeline Mabula kwa Zainab Shomari kupitia ujumbe mfupi wa mtandao wa kijamii wa WhatsApp huku akijua ni uongo.

Katika mashtaka ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu inadaiwa Mei 15, 2022 mkoani Mwanza alijipatia Sh1 milioni kutoka kwa Fauz Abdulrazak akidai zinahitajika na Angeline Mabula.

Mzamiru alidai kuwa katika eneo hilo hilo kati ya Mei 7, 2022 na Juni 22, 2022 mshtakiwa huyo alijipatia fedha kiasi cha Sh 3.5 milioni kutoka kwa Zainab Hamis, akidai kuwa fedha hizo zilihitajika na Angeline Mabula.

Pia inadaiwa alijipatia Sh900,000 kutoka kwa Majid Suleiman, akidai kuwa zinahitajika na Angeline Mabula, huku akitumia laini iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine iliyosomeka Geoffrey John Gabriely.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Swallo alisema kuwa dhamana ya mshtakiwa huyo ipo wazi na kuahirishwa kesi hadi Oktoba 17, 2023 kwa ajili ya hoja za awali.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live