Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aachiwa huru kwa kushtakiwa na sheria isiyotumika nchini

46365 Pic+huru Aachiwa huru kwa kushtakiwa na sheria isiyotumika nchini

Tue, 12 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam imemuachia huru, Isidory Karume (57) aliyekuwa akikabiliwa na shtaka la kukutwa akimiliki risasi mbili baada ya kubainika sheria iliyotumika kumshtaki haipo katika matumizi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hukumu hiyo imetolewa leo na Hakimu Mkazi, Adolf Sachore ambapo upande wa mashtaka uliwakilishwa na wakili wa Serikali, Teddy Mtao.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Sachore amesema Januari Mosi, 2018 Karume ambaye ni mkazi wa Karakata alikuwa akikabiliwa na shtaka la kukutwa akimiliki risasi mbili za bastola bila ya kuwa na kibali.

Kesi hiyo ya jinai namba 40 ya mwaka 2018 iliendeshwa kwa mujibu wa sheria, upelelezi ulikamilika na hatimaye ikaanza kusikilizwa, ambapo upande wa mashtaka uliwaita mashahidi watano.

Mahakama ilipitia ushahidi wa mashahidi  hao wa upande wa mashtaka na mshtakiwa akaonekana ana kesi ya kujibu hivyo naye akatoa ushahidi wake wa kujitetea.

Hakimu Sachore amesema katika kesi hiyo Mahakama iliangalia kama ni kweli mshtakiwa huyo alikutwa akimiliki risasi mbili bila ya kuwa na kibali.

Amesema katika kesi hiyo, Karume anadaiwa kufanya kosa hilo kinyume cha kifungu cha 4(1) na 34(1)(2) cha sheria ya umiliki wa silaha na risasi sura ya 223 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Hakimu huyo amesema mnamo Machi 3, 2015 bunge la Tanzania lilipitisha sheria mpya inayoiwezesha Serikali kudhibiti umiliki wa silaha na risasi. 

Sheria mpya iliyosomwa kwenye bunge na naibu waziri wa mambo ya ndani wakati huo, Pereila Ame Silima inasema mtu atakayekamatwa na silaha za moto kinyume cha sheria atakabiliwa na kifungo cha si chini ya miaka mitano au kulipa faini si chini ya dola 6,000 za Marekani au kuadhibiwa yote mawili.

Sheria hiyo,  mpya pia inadhibiti mambo mbalimbali ikiwamo leseni, umiliki, usafirishaji nje, uingizaji na uuzaji wa silaha. 

Hakimu Sachore amesema kuja kwa sheria hiyo kuliifuta sheria iliyokuwapo awali na kwamba wakati mshtakiwa huyo anatenda kosa hilo kwa mujibu wa hati ya mashtaka Januari 3, 2018 tayari sheria mpya ilikuwa imekwisha anza kutumia.

Hivyo upande wa mashtaka ulitumia sheria ambayo haipo katika matumizi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na akamuachia huru mshtakiwa.



Chanzo: mwananchi.co.tz