Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

3 MBARONI UTOROSHAJI DHAHABU ZA MIL 337/-

Ebf96d7ab157624d729e7e1e6ce5a3a8.jpeg 3 MBARONI UTOROSHAJI DHAHABU ZA MIL 337/-

Thu, 3 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WATU watatu wakiwemo raia wawili wa China wamekamatwa wilayani Ulanga, mkoani Morogoro wakidaiwa kutaka kutorosha madini ya dhahabu yenye uzito wa kilo mbili zinazokadiriwa kuwa na thamani ya Sh milioni 337.

Mkuu wa wilaya ya Ulanga, Ngollo Malenya, aliliambia gazeti hili jana kwa njia ya simu kwamba madini hayo yalichimbwa katika mgodi uliopo katika kijiji cha Isyanga, Kata ya Sali, tarafa ya Ruaha wilayani humo.

Malenya alisema baada ya kupata taarifa walifuatilia na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao Juni 1, mwaka huu, saa 11 jioni katika kijiji hicho.

Bila kuwataja majina, alisema watuhumiwa hao mmoja ni Mtanzania aliyewekeza kwenye uchimbaji wa madini hayo wilayani humo na wawili ni raia China ambao ni wataalamu wa madini.

“Wilaya ya Ulanga ina madini kadhaa lakini wapo baadhi ya wachimbaji hawazingatii kanuni, sheria na taratibu za nchi,” alisema Mkuu wa wilaya huyo.

Alisema ni vyema wachimbaji wanapopata madini wayafikishe katika ofisi za madini zilizopo wilayani humo kwa ajili ya uhakiki kisha utaratibu mwingine uweze kufuatwa.

“Katika hili Serikali tupo macho na hatuwezi kuruhusu udanganyifu wa aina hii, hizi ni mali za Watanzania, mnapopewa leseni muwe waaminifu na hili ndilo Rais Samia Suluhu Hassan anasisitiza ili kuondokana na kero zisizo za lazima,” alisema Malenya.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fotunatus Muslim alithibitisha kukamatwa kwa watu hao na kwamba wanaendelea kuhojiwa.

Chanzo: www.habarileo.co.tz