Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

26 mbaroni wakidaiwa kuchoma moto kituo cha polisi

Pic Moto (600 X 337) 26 mbaroni wakidaiwa kuchoma moto kituo cha polisi

Sat, 23 Sep 2023 Chanzo: Mwananchi

Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora linawashikiliwa watu 26, wakazi wa Kitunda wilayani Sikonge kwa tuhuma za kuchoma moto kituo kidogo cha polisi Kitunda na kufanya uharibifu.

Akizungumzia tukio hilo leo Ijumaa Septemba 22, 2023; kamanda wa Polisi mkoani humo, Richard Abwao amesema watu hao walichoma kituo hicho Septemba 18 mwaka huu chanzo kikiwa mgogoro kati ya askari na mchimbaji madini eneo la Kitunda uliohusu kufunga makarasha.

Abwao amesema askari alikuwa anamweleza mchimbaji kuwa muda wa kufunga makarasha (crushers) kwa lengo la kudhibiti mapato ya Serikali umepita ndipo sintofahamu ilipotokea kati yao na kusababisha mchimbaji kuumia mguu.

Amesema kufuatia hali hiyo wananchi walikasirika kisha kwenda kufanya uharibifu katika kituo hicho kilichojengwa kwa mabati tupu, kukibomoa na kukichoma moto baada ya kuweka miti ndani.

“Watu 26 wamekamatwa juzi (Septemba 20) na tunaendelea na mahojiano nao kuhusiana na tukio hilo,”amesema

Kuhusiana na mchimbaji huyo aliyeumia katika krasha, Kamanda Abwao amesema anaendelea vizuri huku, akidai upelelezi zaidi wa tukio hilo unaendelea.

Chanzo: Mwananchi