Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

26 jela miezi sita kwa ‘kuzamia’ Afrika Kusini

Hukumu Pc Data 26 jela miezi sita kwa ‘kuzamia’ Afrika Kusini

Wed, 11 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewahukumu watanzania 26, kila mmoja kulipa faini ya Sh300, 000 au kwenda jela miezi sita, baada ya kupatikana na hatia ya kuondoka nchini kwenda Afrika Kusini bila kufuata taratibu za uhamiaji.

Waliohukumiwa adhabu hiyo katika kesi ya jinai namba 182/2023 ni Dotto Mkomwa, Yunusi Mzee, Bakari Hassan, Seif Mpingi, Ibrahim Ramadhani, Jumanne Chande na wenzao 20.

Hata hivyo washitakiwa hao wameshindwa kulipa faini na kwenda kutumikia kifungo cha miezi sita jela.

Hukumu hiyo imetolewa leo, Oktoba 11, 2023 na Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Richard Kabate baada ya washtakiwa kukiri kosa lao na mahakakama kutiwa hatiani kwa kosa hilo.

Hakimu Kabate amesema washtakiwa wametiwa hatiani kama walivyoshtakiwa na wamekiri wenyewe shtaka lao, hivyo anawahukumu kila mshitakiwa kulipa faini Sh300, 000 na iwapo watashindwa, basi watatumikia kifungoi cha miezi sita jela.

Awali, Wakili kutoka Idara ya Uhamiaji, Hadija Masoud aliwasomewa hoja za awali, washtakiwa hao ambapo alidia kuwa tarehe na siku isiyojulikana washtakiwa walikwenda Afrika Kusini bila kufuata taratibu za uhamiaji.

Wakili Masoud alidai Oktoba 8, 2023, washtakiwa hao walirudishwa nchini Tanzania wakitokea Afrika Kusini na waliposhuka JNIA, walikamatwa kwa kosa la kuondoka ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania isivyohalali.

Aliiendelea kueleza kuwa washitakiwa hao walidai kuwa walikwenda Afrika Kusini wakitegemea kuwa watapata maisha mazuri na badala yake walikuwa wanazurura huku na kule kwa sababu hapakuwa na nchini humo.

Wakili huyo, alidai baada ya kukamatwa huko Afrika Kusini walirudishwa nchini kwa kutumia ndege ya Serikali na kisha walipelekwa ofisi za uhamiaji mkoa wa Dar es Salaam kwa uchunguzi na mahojiano.

Baada ya kuwasomea maelezo yao, washitakiwa wote walikiri shtaka lao linalowakabili na ndipo walipotia hatiani na kuhukumiwa.

“Mheshimiwa hakimu naiomba mahakama iwape adhabu kali washtakiwa hawa ili iwe fundisho kwa wenzao kwa sababu katika kosa hili, Serikali imegharamika kwa kuchukua ndege ya kuwarudisha nchini, pesa ambayo ingetumika katika shughuli nyingine za kimaendeleo, hivyo tunaomba wapewe adhabu kali," alidai Wakili Masoud.

Kwa upande wa washtakiwa, wao waliomba mahakama iwapunguzie adhabu kwani ni kosa lao la kwanza na hawatarudia tena na kwamba walienda Afrika Kusini kwa ajili ya kutafuta maisha.

Hata hivyo Hakimu Kabate alitupilia mbali ombi la washtakiwa hao la kuwapunguzia adhabu na badala yake aliwahukumi kulipa faini ya Sh300, 000 kila mmoja au kwenda jela mwaka mmoja.

Kabla ya kutoa adhabu hiyo, Hakimu Kabate aliwahoji washtakiwa hao iwapo waliaga familia zao wakati wanaenda Afrika Kusini na majibu yalikuwa kama ifuatayo kwa baadhi ya washtakiwa.

Hakimu: Mshtakiwa Mkomwa uliaga familia yako?

Mkomwa: ndio niliwaga.

Hakimu: Wakasemaje? Uendee tu.

Mkomwa: Kimya.

Hakimu: Ehe mshtakiwa wa pili (Mzee) wewe uliaga familia yako?

Mzee: Hapana

Hakimu: Kwa hiyo uliondoka kama unaenda Temeke?

Mzee: Kimya.

Hakimu: Mshtakiwa wa tatu (Hassan) wewe uliaga familia yako? Au uliruka mazima!

Hassan: Ndio Mheshimiwa niliwaaga

Hakimu: Ehe walikuambiaje?

Hassan: Walinipa Baraka zote

Hakimu: Walikutafutia Passport (Hati ya kusafiria)?

Hassan: Hapana

Hakimu: Ehe mshtakiwa Chichi, wewe uliaga ndugu na familia yako?

Chichi: Ndio niliaga familia kuwa naenda Tunduma, lakini nikajikuta nipo Afrika Kusini.

Hakimu: Unajua ni kosa kisheria?

Chichi: Ndio, Mheshimiwa Hakimu naomba unisamehe nimekosea.

Hakimu: Mshtakiwa Said Njechele, wewe uliaga nani?

Njechele: Niliaga familia nakwenda Mbeya

Hakimu: Na ndugu zako wakafurahi?

Njechele: Kimya

Hakimu: Ukiwaambia unaenda Mbeya utawaletea viazi ma maharage sio?

Njechele: Hapana Mheshimiwa

Hakimu: Mshtakiwa Hamisi Simba, bwana wewe una umri gani?

Mshtakiwa: Nina miaka 47.

Hakimu: Una familia?

Mshtakiwa: Ndio, nina mke na watoto wawili.

Hakimu: Hebu tuambie wewe uliagaje?

Mshtakiwa: Mheshimiwa Hakimu, mimi niliondoka bongo tangu mwaka 2000.

Hakimu: Dar ulikuwa unakaa sehemu gani?

Mshtakiwa: Ubungo Rombo.

Hakimu: Sasa utapakumbuka ulipokuwa unakaa hapo Ubungo?

Mshtakiwa: Kimya.

“Si mnajua Serikali imeingia gharama ya kuwatoa Afrika Kusini na kuwarejesha hapa nchini?” Alihoji Hakimu Kabate na kuongeza

“Ili iwe fundisho kwa watu wengine, mahakama hii inatoa adhabu kama ifuatavyo, najua mmekuja na pesa za kutosha mlizozipata huko Afrika Kusini si ndio? Sasa kila mmoja anatakiwa kulipa faini ya Sh300, 000; ukishindwa unaenda jela miezi sita" alisema Hakimu Kabate.

Hakimu Kabate baada ya kutoa hukumu hiyo, baadhi ya washtakiwa hao walishika vichwa huku wengine wakisikitika na kuanza kuwageukia ndugu zao ambao walikuwa wamekaa katika ukumbu huo wa makahama, huku wakiwauliza kama kama wamekuja na fedha za kuwalipia faini.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo Oktoba 8, 2023 katika uwanja JNIA, uliopo Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam.

Inadaiwa wakiwa raia wa Tanzania, siku hiyo walikamatwa JNIA muda mfupi baada ya kurejeshwa kutoka Afrika Kusini, kwa kosa la kuondoka nchini na kwenda Afrika Kusini.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuondoka Tanzania kinyume cha sheria na bila kufuata sheria za uhamiaji.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live