Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

23 kortini wizi wa Sh mil 780 NMB Mbezi

568cbcb3c5ac328e5d085e4584334aae 23 kortini wizi wa Sh mil 780 NMB Mbezi

Mon, 11 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakazi 23 wa Dar es Salaam, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka nane likiwemo la wizi wa Sh milioni 780 katika tawi la Benki ya NMB Mbezi Beach.

Washitakiwa hao ni Menjestu Mselema(44), Tulipo Mwakuzi(40), Bernard Machimbo, Joseph Mwatonoka, Juma Mbulinda, Joseph Mpondo maarufu kama Khomango, Jabiri Mgoli, Englibert Masare, Beda Mmari, Kaisi Nasibu, Bernadetha Mwakuzi na Godwin Erio.

Wengine ni Anold Erio, Agnes Mselema, Florah Mwita, Oswald Mselema, Olaph Mselema, Janeth Shilla, John Mkamba, Edes Hyera, Sylidion Odilo, Said Mkimu na Grace Komba.

Washitakiwa hao wamesomewa mashitaka yao na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ester Martin akisaidiana na Wakili wa Serikali, Timotheo Mmari, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ramadhani Rugemalira.

Akisoma mashitaka hayo, Mmari amedai katika mashitaka ya kwanza, washitakiwa kwa pamoja wanadaiwa kati ya Juni Mosi , 2020 na Juni 8, 2020 katika Jiji la Dar es Salaam walikula njama za kutenda kosa la wizi.

Katika mashitaka ya pili, washitakiwa wote wanadaiwa Juni 8, 2020, katika benki ya NMB tawi la Mbezi Beach, walijipatia Sh milioni 780 mali ya Kampuni ya SGA.

Katika mashitaka ya tatu ya utakatishaji fedha, linalowakabili washitakiwa 20, isipokuwa mshitakiwa Odilo, Mkimu na Komba, wanadaiwa Juni 8, 2020 na Agosti 31, 2020 katika jiji la Dar es Salaam, walijipatia Sh milioni 780, wakati wakijua fedha hizo ni zao la kosa tangulizi la wizi.

Pia inadaiwa Julai Mosi 2018 na Mei 30, 2020 katika maeneo tofauti ya Makambako mkoani Njombe mshitakiwa Mwakuzi kwa lengo la kuficha uhalali wa fedha, alitumia sehemu ya Sh milioni 780 kwa kununua pikipiki moja, wakati akijua fedha hizo ni kosa tangulizi la wizi.

Inadaiwa siku na eneo hilo, Mwakuzi kwa lengo la kuficha uhalali wa fedha anazodaiwa kuiba, alitumia sehemu ya fedha hizo kwa kununua Power Tiller, wakati akijua fedha hizo ni kosa tangulizi la wizi.

Wakili Mmari alidai mashitaka ya sita ni ya kutakatisha fedha, yanayomkabili Mwatonoka. Anadaiwa Mei 20, 2020 katika maeneo ya Chimala mkoani Mbeya, kwa lengo la kuficha uhalali wa fedha, mshitakiwa huyo alitumia sehemu ya Sh milioni 780 kwa kununua magunia 910 ya mpunga yenye thamani ya Sh milioni 47.2, wakati akijua fedha hizo zinatokana na kosa tangulizi la wizi.

Katika mashitaka ya saba, Mpondo anadaiwa kutenda kosa la kutakatisha fedha kati ya Julai Mosi na Mei 30, 2020 katika eneo la Ikungi mkoani Singida, kwa lengo la kuficha uhalali wa fedha kwa kutumia sehemu ya Sh milioni 780 anazodaiwa kuiba na kununua kiwanja chenye thamani ya Sh milioni nne.

Inadaiwa siku na eneo hilo la Ikungi mkoani Singida, Mpondo kwa nia ya kuficha uhalali wa fedha, alitumia sehemu ya fedha hizo kununua kiwanja kingine chenye thamani ya Sh milioni tatu.

Baada ya kusomewa mashitaka yao, Wakili Martin amedai kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) amewasilisha hati ya kuruhusu mahakama hiyo kusikiliza shauri hilo.

Hata hivyo, upande wa mashitaka umedai kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea washitakiwa maelezo ya awali.

Hakimu Rugemalira baada ya kusikiliza maelezo hayo, ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 21, 2022 kwa ajili ya kusomewa hoja za awali.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live