Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

22 jela miezi sita kwa kwenda Afrika Kusini bila kufuata taratibu

93007 Pic+bondeni 22 jela miezi sita kwa kwenda Afrika Kusini bila kufuata taratibu

Fri, 24 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu kifungo cha miezi sita jela washtakiwa 22 baada ya kuwakuta na hatia ya kuondoka Tanzania kwenda Afrika Kusini bila kufuata taratibu.

Washtakiwa hao ni Mzazuri Mohamed, Mohamed Said, Masoro Musa, Mneka Mehra, Kabila Hussein, Ally Hassan, Jamalino Rashid, Abadi Nassoro, Waziri Adam, Said Salum na Chuwa Sadiki.

Wengine ni Salim Kassim, Macalot Alex, Kayeng Winston, Idali Charles, Ibrshim Mohamed, Jafari Zebra, Omare Fizo, Mbuna Edson, Ulembo Azide, Fizo Charles na Mnangwa Rajabu.

Akisoma hukumu hiyo leo Ijumaa Januari 24, 2020 hakimu mwandamizi wa mahakama hiyo, Vicky Mwaikambo amesema washtakiwa hao wamekiri kutenda kosa hilo, mahakama imewapa adhabu ya kifungo.

Hakimu huyo amesema washtakiwa hao wana nguvu ya kufanya kazi, wanatakiwa kwenda gerezani kutumia nguvu hizo kufanya kazi.

"Nikiwatazama wote ni vijana mnaweza kufanya shughuli za kujenga Taifa na mna nguvu lakini mmeamua kuiingizia Serikali hasara,  mmesafirishwa  na ndege (kutoka Afrika Kusini hadi Tanzania), kutokana na hilo ninawahukumu kwenda jela miezi sita,” amesema Mwaikambo.

Pia Soma

Advertisement

Awali wakili wa Serikali, Shija Sitta amedai haoni sababu ya washtakiwa hao kwenda Afrika Kusini  kwa madai kuwa kitendo hicho kimeidhalilisha Tanzania kwa sababu hakuna walichopata walipokuwa ugenini.

"Naiomba mahakama iwape adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia hizo," amedai Sitta.

Katika kesi ya msingi Januari 21, 2020 katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) washtakiwa hao walikamatwa baada ya kurejeshwa nchini wakitoka Afrika Kusini walikokwenda bila kufuata taratibu.

Wakati huohuo, wenzao 20  wamefikishwa katika mahakama hiyo wakikabiliwa na kosa kama hilo.

Akisoma hati ya mashtaka wakili Sitta amedai washtakiwa hao walikamatwa JNIA wakitokea Afrika Kusini walikokwenda bila kufuata taratibu.

Baada ya maelezo hayo washtakiwa hao walikiri kutenda kosa hilo.

Hakimu Mwaikambo amesema shauri hilo litasikilizwa Januari 27, 2020 kwa kuwa lipo kwa  Hakimu mwandamizi, Augustina Mmbando ambaye amepata udhuru

Chanzo: mwananchi.co.tz