Jeshi la Polisi limesema linawashikilia watu zaidi ya 20 kutokana na mapigano ya wakulima na wafugaji yaliyotokea juzi katika Kata ya Kibirashi wilayani Kilindi Mkoa wa Tanga na kusababisha vifo vya watu sita.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na wananchi wa kijiji cha Elerai wilayani Kilindi wakati akiwa kwenye ziara ya kufuatilia tukio la mapigano ya wakulima na wafugaji yaliofanyika vijiji vya Elerai, Kibirashi na Ngaroni.
Alisema watu zaidi ya 20 wanashikiliwa na jeshi hilo huku juhudi za kuwasaka wengine waliohusika zikiendelea.
Sirro aliongeza kuwa kutokana hali ya wasiwasi walionayo wananchi katika maeneo hayo, pia amepeleka vikosi maalumu vya jeshi hilo kwa ajili ya kulinda amani ya wananchi wa kata hiyo ya Kibirashi
“Niwahakikishie wananchi wote wa eneo hili kuwa waishi kwa amani, nimeguswa na tukio hili wakati ninawasili kuna wanafunzi wameniambia leo (jana) hawajakwenda shule wanaogopa kuuawa. Hii sio sawa kabisa, lazima wote waliohusika wakamatwe, vikosi vipo kutoka makao makuu mkoani na Morogoro kwa ajili ya kuwalinda,” alisema IGP Sirro.
Hata hivyo, Sirro alitoa nafasi kwa wale waliohusika kujisalimisha polisi na endapo hawatafanya hivyo jeshi la polisi litawatafuta popote walipo.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima kwa upande wake, alipiga marufuku wanananchi kuleta masuala ya udini na ukabila yanayoendelea, kwa sababu imebainika kuwa wapo wananchi wanataka kujitenga na wenzao kwa kujiwekea maeneo maalumu, kitu ambacho ni makosa.
Malima alisema zipo taarifa kuwa wananchi wa Elerai, Kibirashi na Ngaroni wamejiyenga tabia kwamba kila mmoja eneo aliopo ni lake, hivyo hakuna mwingine kuingia kitu ambacho ni kinyume na utaratibu.
Ayoub Haji, mkazi wa eneo hilo alisema mgogoro huo ni wa zaidi ya miaka 20, ila kila kiongozi anayefika kuchukua hatua, hakuna majibu yanayorudi hivyo kusababisha mgogoro huo kuendelea.
Alisema kuwa pia wapo askari wanakamata wafugaji, lakini baadaye hakuna hatua inayochukuliwa dhidi yao na badala yake kuachiwa kitendo ambacho kinaongeza chuki kwenye jamii.
“Huu mgogoro ulianza zaidi ya miaka 20 na hao wenye silaha walishaorodheshwa na majina yao kupelekwa wilayani, ila mpaka sasa hakuna hatua iliyochukuliwa na tatizo lingine wapo askari polisi wamekaa muda mrefu kwenye eneo hilo nao wanahusika,” alisema Haji.
Aidha, Maria Daud, mkazi wa Elerai alieleza kuwa shida kubwa pia hakuna njia ya kupitisha mifugo, hivyo wengi kupitisha kwenye njia ambazo sio rasmi, hali inayochangia kuleta matatizo kwenye jamii.