Watu 20, akiwamo Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha, Ndirango Senge Laizer wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha wakikabiliwa na shtaka la mauaji ya kukusudia ya askari polisi, Garlus Mwita Garlus.
Garlus (36) aliuawa Juni 10, 2022 huko Loliondo kwa kuchomwa mkuki na watu wasiojulikana wakati yeye na askari wenzake walipokuwa wakiimarisha usalama kwenye kazi ya uwekaji wa alama za mipaka.
Mipaka hiyo inawekwa katika eneo la Pori Tengefu la Loliondo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 1,500 ambalo limetengwa kwa ajili ya shughuli za uhifadhi na vyanzo vya maji na ni la mazalia ya wanyama.
Mbali na mwenyekiti huyo, wengine waliofikishwa mahakamani ni pamoja na madiwani wanaotokana na CCM wa kuchaguliwa na wa viti maalumu kutoka kwenye baadhi ya Kata za Loliondo.
Taarifa zilizotufikia kutoka mahakamani hapo jana, zilieleza kuwa watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani juzi na taarifa za kufikishwa kwao zilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii jana asubuhi.
Watuhumiwa wengine wanaodaiwa kushtakiwa pamoja na mwenyekiti huyo ni Molongo Pachal, Albert Selembo, Simeli Parwat, Lekayoko Parmwati, Sapati Parmwati, Ingoi Kanjwel, Sangai Morongeti, Morijoi Parmati na Morongoti Meeki.
Kulingana na hati ya mashtaka ambayo nayo pia ilisambaa mitandaoni, wamo pia Shengena Killel, Kambatai Lulu, Moloimeti Yohana, Ndirango Laizer, Joel Lessonu, Simon Orosikiria, Damian Laiza, Mathew Eliakimu, Luka Kursas, Talengo Leshoko na Kijoolu Kakeya.
Imeelezwa watuhumiwa hao walipofikishwa mahakamani hapo walisomewa mashtaka hayo na baadaye kupelekwa gereza Kuu la Kisongo lililopo Jijini Arusha kwa kuwa tuhuma za mauaji zinazowakabili hazina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, haikufahamika kama wanakabiliwa na mashtaka mengine, baada ya waandishi waliokuwa wakifuatilia kujua undani wa tukio hili kukosa ushirikiano wa kupata nyaraka za kimahakama.
Mbunge azungumza
Mbunge wa Ngorongoro (CCM), Emmanuel Ole Shangai alipozungumza na Mwananchi kutaka kujua kama anazo taarifa juu ya kesi hiyo alijibu kuwa; “Tunafuatilia suala hilo na tayari kuna wanasheria nao wanafuatilia kujua kile kilichotokea Mahakamani.”
Hata hivyo, Mkurugenzi wa shirika moja lisilo la kiserikali mkoani Arusha ambaye aliomba kuhifadhiwa jina, alithibitisha kufikishwa mahakamani kwa viongozi hao wa kisiasa pamoja na baadhi ya wananchi.
“Ni kweli wamefikishwa mahakamani jana (juzi), lakini hatujui kwa kina kilichotokea kwa sababu walikuwa hawana mawakili kutokana na taarifa za kufikishwa mahakamani kutopatikana,” alisema mkurugenzi huyo.
Kabla ya kufikishwa kortini hiyo juzi, Mbunge Ole Shangai alikaririwa akitoa taarifa ya kutojulikana walipo viongozi 10 wa wilaya hiyo, akiwemo Mwenyekiti wa CCM na madiwani hao ambao wote wamefikishwa mahakamani.