Jeshi la Uhamiaji nchini Tanzania limewatia mbaroni raia wa kigeni 20, 063 kwa tuhuma za kuingia nchini kinyume cha Sheria katika kipindi cha miezi minane iliyopita.
Kwa mujibu wa Kamishna wa Uhamiaji (Fedha na Utawala), Hamza Ismail Shaban, wageni hao wamekamatwa kati ya Julai, 2022 hadi Machi, 2023 na tayari watu 13, 281 wamerejeshwa nchini mwao huku taratibu za kisheria zikiendelea kwa waliosalia.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuzinduzi jengo la ofisi za Uhamiaji Mkoa wa Geita ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yanayofanyika Aprili 26 kila mwaka, Shaban amesema watu hao walinaswa kupitia operesheni za kila mara za kuwasaka raia wa kigeni wanaoingia nchini kinyume ha sheria.
Paspoti kielektroniki
Akizungumzia maboresho ya huduma, Afisa huyo wa Uhamiaji amesema taasisi hiyo ya umma inaendelea kuboresha huduma zake kupitia Uhamiaji mtandao unaowezesha Watanzania kupata hati za kusafiria kielektroniki.
“Maboresho haya tayari umewezesha Watanzania 92,154 kupata hati za kusafiria kupitia huduma ya Paspoti Kielektoniki,” amesema Shaban
Amesema maboresho hayo pia yamewezesha Uhamiaji kutoa Visa 767, 584 kwa wageni kutoka mataifa mbalimbali walioingia nchini kwa shughuli mbalimbali ikiwemo utalii.
“Uhamiaji pia tumetoa vibali vya ukaazi kwa wageni 12, 608 walioingia nchini kwa shughuli mbalimbali ikiwemo uwekezaji,” amesema
Akizungumzia uzinduzi wa jengo jipya la ofisi ya Uhamiaji Geita, Shaban amesema jengo hilo lililogharimu zaidi ya Sh2.5 bilioni lililoanza kujengwa mwaka 2015 utatoa fursa kwa wananchi kupata huduma zote za uhamiaji ikiwemo maombi na utoaji wa hati za kusafiria, hati za dharura na vibali vya ukaazi katika eneo moja.
Mkurugenzi wa Malalamiko kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Kamishna wa Polisi, Albert Nyamhanga amesema Serikali imetenga zaidi ya Sh12.2 bilioni kwa Jeshi la Uhamiaji kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa mwaka 2023.
Amesema katika mikakati hiyo, Serikali pia imetenga zaidi ya Sh70 bilioni kutekeleza miradi ya maendeleo kwa ajili ya yyombo vingine vya usalam vilivyoko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ikiwemo Jeshi la Polisi, Magereza na Zimamoto na Uokoaji.
Akizindua jengo hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Sera, Uratibu na Baraza la Uwakilishi Zanzibar, Hamza Hassan Juma amesema Serikali inatambua na kujivunia mafanikio yanayopatikana kupitia Jeshi la Uhamiaji huku akiuagiza uongozi wa taasisi hiyo kuendeleza ubunifu kuboresha huduma, hasa zinazotolewa kielektroniki kutokana na maendeleo ya Sayansi na Teknolojia.
“Maofisa Uhamiaji mnao wajibu wa kufanya kazi kwa weledi na ubunifu huku mkizingatia sheria, kanuni na miongozo,” amesema Hamza
Waziri huyo ameutaka uongozi wa Uhamiaji kuwachukulia hatua stahiki za kinidhamu na kisheria maofisa wote wanaobainika na kuthibitika kukiuka sheria, kanuni na miongozi, hasa wanaoharibu taswira ya taasisi na Taifa kwa kuwabughudhi wageni, wawekezaji na kujihusisha na vitendo vya rushwa.