Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

160 mbaroni kwa tuhuma mbalimbali, zipo za mauaji

Musoma Polisiiiiiii.jpeg 160 mbaroni kwa tuhuma mbalimbali, zipo za mauaji

Sat, 10 Jun 2023 Chanzo: Mwananchi

Jeshi la Polisi mkoani Mara linawashikilia zaidi ya watu 160 kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo mauaji na unyang'anyi wa kutumia silaha huku 11 wakituhumiwa kwa matukio ya mauaji ya boda boda wanne na kujeruhi watu watatu kwa kuwakata mapanga Wilaya ya Butiama mkoani humo.

Taarifa hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Salim Morcase leo Ijumaa Juni 9, 2023 ambapo amesema watu hao wamekamatwa kufuatia oparesheni iliyofanywa na jeshi hilo kuanzia Mei 3 hadi Juni 8 mwaka huu. “Kati ya hao watu 11 waliohusika na matukio haya makubwa mawili ya mauaji ya boda boda na majeruhi wa mapanga kule Butiama watuhumiwa wawili ni wanawake na wote ushahidi unaonyesha wameshiriki kwenye matukio hayo lakini pia tumewakamata na silaha mbalimbali walizokuwa wakitumia kwenye uhalifu huo ikiwemo bastola moja aina ya Browing,” amesema

Usiku wa Mei 21, 2023 katika vijiji vya Nyamikoma na Nyakiswa wilayani Butiama boda boda wanne waliuwawa kwa kukatwa katwa mapanga na miili yao kutelekezwa sambamba na pikipiki zao katika vichaka vilivyo pembeni ya barabara iendayo katika kijiji cha Nyakiswa. Pia Usiku wa Juni Mosi mwaka huu watu watatu walijeruhiwa kwa kukatwa katwa mapanga baada ya watu wasiojulikana kuvamia nyumba moja yenye duka, vyumba vya kulala wageni na baa katika kijiji cha Bisumwa Wilaya ya Butiama. Amesema kufuatia oparesheni hiyo jeshi hilo limeweza kudhibiti matukio makubwa ya kiuhalifu yakiwemo ya mauaji yaliyaonza kukithiri hasa katika wilaya ya Butiama. Kamanda Morcase ameongeza kuwa, miongoni mwa watu wanaoshikiliwa ni pamoja na Joel Daudi mkazi wa Arusha aliyekamatwa akiwa na sare za jeshi la polisi jozi tatu, kofia mbili zenye nembo ya polisi, mikanda mitatu ya polisi pamoja na pingu. "Tulipomuhoji alikiri kutumia vitu hivyo kwenye matukio mbalimbali ya uhalifu mkoani Arusha na hapa Mara, tunakamilisha uchunguzi ili aweze kufikishwa mahakamani," amesema Amesema oparesheni hiyo pia ilihusisha masuala ya usalama barabarani ambapo watu 72 wamekamatwa kwa kuvunja sheria za usalama barabrani ikiwa ni pamoja na kuendesha vyombo vya moto bila kuwa na leseni huku 37 kati yao wakiwa wamefikishwa mahakamani ambapo mmoja amefungwa na wengine kulipa faini. "Makosa mengine yalihusu madawa ya kulevya ikiwemo bangi, gongo, nyara za serikali pamoja na kupatikana na mali za wizi ikiwemo pikipiki sita,simu 14 za mkononi na vitu vingine,"amesema Kamanda Morcase

Chanzo: Mwananchi