Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

15 kizimbani wakidaiwa kutumia simu kutapeli

Ed5ac48adfbb09d74a8618a87efba196.jpeg 15 kizimbani wakidaiwa kutumia simu kutapeli

Thu, 23 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAKAZI 15 wa wilaya ya Kilombero Morogoro wamefi kishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka ya kula njama kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutumia laini za watu wengine bila kutoa taarifa.

Washitakiwa hao ni mkulima Meniad Ndiyo (25), dereva bodaboda, Dotto Likumbai (29) , mkulima Abdallah Migoi (26) na mawakala Athumani Roho (28) na Onesmo Ngajela (24) . Walisomewa mashitaka 10 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi. Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Yusto Ruboroga wakulima Saidi Sevenjari maarufu ‘Dangote’ (35) na Hasani Njalatango (34) walisomewa mashitaka sita.

Wafanyabiashara Filbert Ngatunga (26), Octavian Lekaleka (26) na madereva wa bodaboda Francis Mhombera (24) na Moses Mhindi (25) walisomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate.

Mawakala Michael Ngalami (21) na Omary Mbena (31), wanakabiliwa na mashitaka saba mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Agustina Mbando. Dereva wa pikipiki, Rashid Mshamu (23) na wakala Emmanuel Assey (19), wanakabiliwa na mashitaka sita mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rashidi Chaungu.

Akisoma mashitaka, Wakili wa Serikali, Jacqueline Nyantori alidai kuwa washitakiwa Sevenjari na Njalatango kati ya Januari Mosi na Juni 15, 2020 maeneo mbalimbali wilayani Kilombero, kwa pamoja walikula njama kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Pia alidai mshitakiwa Sevenjari alituma ujumbe mfupi wa maandishi, ukionesha kwamba Sh 300,000 zimepokewa kupitia Airtel money kutoka kwa Antony Ngonyani Juni 22 mwaka huu saa mbili asubuhi, hivyo salio ni 750,000/-.

Dangote anadaiwa alijipatia Sh 2,132,980 kutoka namba mbalimbali kwa kudanganya kwamba fedha hizo, zimetumwa kimakosa arudishiwe. Nyantori alidai Mei 22 mwaka huu maeneo ya Ifakara, kwa kupitia mfumo wa kompyuta mshitakiwa huyo alisambaza ujumbe kuonesha Ngonyani alipokea Sh 300,000 na salio lake ni 750,000 na kwamba fedha hizo zimetumwa kimakosa hivyo arudishiwe.

Washitakiwa hao pia wanadaiwa kushindwa kutoa taarifa kuhusu mabadiliko ya laini ya simu kosa walilolitenda Januari Mosi na Juni 15 mwaka huu maeneo ya Kilombero, na walitumia namba za simu zilizosajiliwa kwa majina ya watu wengine bila kutoa taarifa kwa mtoa huduma. Washitakiwa walikana mashitaka na walirudishwa rumande.

Chanzo: habarileo.co.tz